Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar – TAMWA ZNZ, kimeziomba taasisi zinazosimamia masuala ya sheria na upatikanaji wa haki likiwemo Jeshi la Polisi, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Mahakama, kuendeleza uwazi na mawasiliano katika kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia ikiwemo mauaji.
Hatua hiyo inakuja kufuatia hivi karibuni Mahakama Kuu Zanzibar kutoa taarifa kuwa imemuhukumu mshitakiwa Haji Jaha Issa (37), kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kumuua kwa makusudi Hajra Abdallah
Abdallah (21), kwa kumchoma kisu, iliyotolewa na Jaji Rabia Hussein Mohammed ambaye aliridhishwa na ushahidi uliotolewa katika mauaji hayo yaliyofanyika februari 26, 2020 Paje, Mkoa wa kusini Unguja.
Kupitia taarifa yake iliyosainiwa na Mkurugenzi wa TAMWA – ZNZ, Dkt. Mzuri Issa imeeleza kuwa inaamini uwazi na utoaji taarifa kwa Mahakama ni msingi mzuri wa utawala bora na kwamba itaongeza imani kwa wananchi katika kutegemea hukumu za vyombo vya sheria na pia kupunguza kiwango cha uhalifu kwa vile kitawatisha wanaotaka kutenda makosa hayo na kwamba inategemea kuwa Mahakama pamoja na vyombo vingine vya sheria vitaweka wazi taarifa zake kuhusu mashitaka na hukumu, ili kufikia matakwa hayo ya nchi na ya kidunia.
Aidha, taarifa hiyo pia imefafanua kuwa ni aula pia kwa taasisi hizo kutoa taarifa za kila mwezi kuhusiana na mwenendo wa kesi na kueleza mafanikio na changamoto zake na kuweka mifumo ya kuripoti malalamiko ambapo kwa mujibu wa rekodi ya TAMWA ZNZ, jumla ya wanawake 19 na watoto wanne (4)
wameuawa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar tokea mwaka 2016 hadi Mei 2023 na Mei 2023 Wasichana wawili Laura Msemwa (23) na Khairat Juma Bakari (28) waliuwawa kikatili huko Bububu Kijichi na Mbuzini Wilaya ya Maghari “A” Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
“Tunaomba pia Mahakama na taasisi nyengine husika kuendelea kutoa taarifa za kesi zilizosaliana hivyo kuongeza amani na ustawi kwa maisha ya wanawake na watoto ambao mara nyingindio wanaoathirika katika vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia.TAMWA ZNZ inatoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na mihimili hii muhimu ilikuharakisha na kufanikisha uchunguzi wa makosa ya kihalifu na hatimae haki itendeke,” ilizidi kueleza taarifa hiyo.