Wazazi na Walezi wa Kata ya Kitanga Wilayani Kasulu, wameonywa juu ya kuwatumikisha watoto katika shughuli za kiuchumi, ikiwemo ufugaji wakati wa muda wa masomo na kupelekea watoto hao kukosa haki ya msingi ya kupata elimu.
Onyo hilo, limetolewa na Polisi Kata ya Kitanga Mkoani Kigoma, Mkaguzi wa Msaidizi wa Polisi, Titus Mwangomale wakati akitoa elimu ya malezi bora kwa watoto.
Amesema, wazazi na walezi kwa mujibu wa sheria ya mtoto wanapaswa kuwapa watoto wao mahitaji muhimu ikiwemo chakula, mavazi, elimu, matibu na kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili.
Aidha, Mwangomale ameongeza kuwa kuwatumia watoto katika shughuli za kiuchumi muda wa masomo kwenye kazi za ufugaji ni chanzo cha utoro shuleni, hivyo jamii inapaswa kuwapa haki za msingi ikiwemo elimu kwani wao ni taifa la kesho.