Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka wadau mbalimbali wanaohusika na mapambano dhidi ya UKIMWI nchini kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania – TACAIDS, kuhakikisha kuwa wanatenga fedha za kutosha kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI nchini badala ya kutegemea wafadhili kwa kiasi kikubwa.

Dkt. Biteko amesema hayo wakati wa Mkutano Maalum wa Wadau wanaoshughulikia Udhibiti wa UKIMWI Tanzania uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2023 mjini Morogoro na kuhusisha viongozi wa Serikali, Wadau wa Maendeleo na Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI.

“Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI na nawataka TACAIDS na wadau kuhakikisha mnashirikiana kwa pamoja dhidi ya mapambano ya Ukimwi kwa kuongeza ushiriki wa wananchi pia” Amesisitiza Dkt. Biteko.

Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Tanzania, kupitia Serikali ya Awamu ya Sita, imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali katika mapambano dhidi ya UKIMWI ambayo yamepelekea kupungua kwa maambukizi mapya, kupungua kwa idadi ya vifo vinavyotokana na UKIMWI, mwamko wa watu wanaotumia dawa (ARV) umeongezeka, maambuki ya Mama kwenda kwa mtoto yamepungua huku lengo likiwa ni kutokuwa na vifo vinavyotokana na UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

“Tumeshuhudia pia unyanyapaa dhidi ya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi ukipungua, na haya yote yanatokea huku kukiwa na ushirikiano wa Wadau, hivyo nawapongeza nyote kwa juhudi zenu,” Amesema Dkt. Biteko.

Ameeleza kuwa, pamoja na juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali pamoja na Wadau, bado UKIMWI haujadhibitiwa inavyotakiwa, hali inayoweza kupelekea maambukizi mapya kuongezeka hivyo ametaka wadau wote wanaohusika kuendelea na juhudi za utoaji afua mbalimbali zenye lengo la kumaliza UKIMWI.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dkt. Jerome Kamwela amesema kuwa, Mkutano huo unalenga kutoa nafasi ya mashaurinao kati ya Serikali na Wadau wake katika mapambano dhini ya UKIMWI, na kwamba Mkutano huo ni muhimu wakati Tanzania ikielekea kufikia lengo la dunia la kumaliza UKIMWI ifikapo mwaka 2030 ambapo inatakiwa kusiwe na maambukizi mapya ya UKIMWI, kusiwe na vifo vinavyotokana na UKIMWI pia, kusiwe na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.

Amesema, Mkutano huo unaangalia usimamizi na uwajibikaji wa pamoja kati ya Wadau na Serikali, kuangalia uendelevu wa kifedha na rasimali, kuangalia uendelevu wa program za huduma pia mkutano huo utawawezesha wadau kujadiliana mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza katika mapambano dhidi ya UKIMWI na namna ya kuzitatua.

Viongozi waliohudhuria Mkutano huo maalum ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Joyce Ndalichako na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na UKIMWI, Stanslaus Nyongo na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima.

Dirisha Dogo - Azam FC kuhamia Kenya
Mo Salah: Ninamtamani Kevin De Bruyne