Lydia mollel – Morogoro.

Katika kuelekea kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani, ambacho hufanyika Desemba Mosi kila mwaka, Viongozi wa dini nchini wametakiwa kuwaelimisha na kuwajenga Vijana katika maadili mema, ili kuwaepusha na maambukizi ya VVU .

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ameyasema hayo wakati ufunguzi wa Mdahalo kati ya Vijana na Viongozi wa dini uliofanyika mkoani Morogoro, ili kudhihirisha jitihada za pamoja kati ya Taasisi za dini na Serikali katika kulinda na kuhamasisha vijana kutambua hali zao za maambukizi ya VVU na kupata elimu ya  Afya ya Uzazi.

Amesema Takwimu zinaonesha kuwa moja ya makundi yaliyo nyuma katika kufikia malengo yaliyowekwa  ya Sifuri tatu ni kundi la VIJANA,Kwani pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kwenye afua za VVU na UKIMWI, vijana wengi wenye umri wa miaka 15-24 hawajui hali zao za maambukizi ukilinganisha na watu wenye umri mkubwa.

“Maambukizi mapya yameendelea kushuka mwaka hadi mwaka, Na hadi sasa takwimu zinaonesha kuwa takribani watu 54,000 waliambukizwa VVU mwaka 2021 nchini ambapo ni  sawa na takribani watu 4,500 kwa mwezi au watu 150 kwa siku,” amesema Dkt. Yonaz.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo amebainisha kuwa baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika mapambano dhidi ya UKIMWI kwa vijana kuwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wa Dini kuwazuia watu wanaoishi na VVU kutumia dawa za kufubaza makali ya virusi kutokana na imani kwamba maombi pekee au uponyaji wa kimiujiza pekee ndivyo vinavyokubalika.

“Baadhi ya watu wanaoishi na VVU huacha matibabu kutokana na mafundisho na matamko ya baadhi ya viongozi wa Dini, Baadhi ya viongozi wa Dini kutotoa tahadhari ya kutosha kuhusu mahitaji maalum ya vijana wanaoishi na VVU na changamoto wanazokumbana nazo zinazohusiana na matibabu,” Amesema Dkt. Jim Yonazi.

Aidha, ametoa rai kwa viongozi wa Dini kutumia majukwaa yao kutoa elimu ili kusaidia kuhamasiaha waumini na jamii  katika mwitikio  mzuri wa kutumia dawa,kupata matibabu ,kuhamasisha upimaji na kusaidia katika mapambano dhidi ya unyanyapaa, ubauguzi na ukatili wa kijinsia.

Ikumbukwe kuwa maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani hufanyika kila mwaka, ambapo mwaka huu Kitaifa yatafanyika mkoani Morogoro Disemba Mosi chini ya kauli mbiu isemayo “JAMII IONGOZE KUTOKOMEZA UKIMWI.”

Benchikha anataka makombe Simba SC
Mwalimu jela maisha kwa kumlawiti Mwanafunzi