Bondia wa ngumi za kulipwa Twaha Kassim ‘Kiduku’ ameingia kambini mjini Morogoro kujiandaa na pambano la kufunga mwaka litakalofanyika Desemba 26, mwaka.

Kiduku atapanda ulingoni kuzichapa na Mohamed Sebyala kutoka Uganda katika pambano lisilo la Ubingwa la raundi 10, uzito wa juu, litakayofanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es salaam.

Kocha wa Bondia huyo, Pawa Iranda amesema kambi ya Kiduku itamuwezesha kufanya mazoezi magumu ikiwemo kukimbia na kupanda katika Milima mirefu iliyopo Morogoro.

Iranda amesema, pia Kiduku atafanya mazoezi ya kuongeza pumzi na stamina lengo likiwa kujiweka fiti kumvaa mpinzani wake.

“Kabla ya kuingia kambini, Kiduku alifanya mazoezi mepesi ya kuuweka mwili sawa na sasa ni wakati wa kufanya mazoezi magumu na kujiweka fiti kwa asilimia 100 kupambana na Sebyala,” amesema.

Kocha huyo amesema atamuongoza bondia wake kujiandaa kikamilifu na kushinda pambano, lengo likiwa kuumaliza mwaka 2023 vizuri.

Akizungumzia kambi, Kiduku amesema yupo tayari kufanya mazoezi makali yatakayorudisha kiwango chake na kufanya vizuri katika pambano linalofuata.

Kiduku amesema anataka kushinda pambano dhidi ya Sebyala na kurudisha heshima baada ya kudundwa katika mapamnbano mawili mfululizo kimataifa yaliyopita.

Promota wa pambano, Meja Selemani Semunyu, amesema pamoja na pambano hilo, kutakuwa na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii wa Bongo fleva na singeli.

Kiduku Atapanda ulingoni kumkabili Sebyala huku akiwa na kumbukumbu ya kupoteza pambalo lililopita kwa pointi baada kupigwa na Asemahle Wellem kutoka Afrika Kusin, katika pambano lililofanyika Julai 30, mwaka huu jijini Mwanza.

Makala: Mvua za El-nino na upande wa pili wa shilingi
Simba SC yamaliza dakika 540 kimataifa