Taarifa za vifo vya takriban watu 49 na wengine zaidi ya 90 kujeruhiwa kufuatia maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mafuriko yaliyotokana na Mvua za El-nino katika Mkoa wa Manyara kaskazini mwa Tanzania yameleta simanzi na kuacha majonzi kwa familia za waathiriwa, jamii ya watu wa Manyara na Watanzania kwa ujumla.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga huku anasema idadi hiyo ya vifo huenda ikaongezeka, huku Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Janeth Mayanja akisema mvua kubwa iliyonyesha Jumamosi (Desemba 2, 2023), katika mji wa Katesh, ilisababisha athari za barabara nyingi katika eneo hilo kutopitika kwani zilizongwa na tope la udongo, miti na mawe yaliyosombwa na mafuriko hayo.

Hali hii ilipelekea taharuki kwa wakazi wa maeneo hayo na nchimni kiujumla ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akatuma salamu za rambirambi na kusema uwepo wa juhudi zaidi za Serikali utazingatiwa ili kuokoa maisha ya watu na mali zao.

Ifahamike kuwa awali Shirika la Sayansi la Marekani – NOAA, Shirika la Hali ya Hewa Ulimwenguni – WMO na Umoja wa Mataifa walitangaza ujio wa mvua hizi na kila nchi kupitia Mamlaka za hali ya Hewa zilitoa taarifa za tukio hilo la asili ambalo hutokea kila baada ya miaka kadhaa kufuatia kuonekana kwenye mifumo ya hali ya hewa.

Wanasayansi wanasema El-nino pia huchochewa na ongezeko la joto duniani kote na kusababisha ukame na mvua kubwa katika baadhi ya maeneo huku wakihofia huenda ikashuhudiwa uwepo wa athari zaidi mwishoni mwa mwaka 2023 hadi mwakani 2024 kama inavyojidhihirisha.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya hali ya hewa Nchini – TMA, El-Nino ni mfumo wa hali ya hewa unaosababishwa na uwepo wa joto la bahari la juu ya wastani katika eneo la kati la kitropiki katika Bahari ya Pasifiki. Hali hii kwa kawaida huambatana na vipindi vya mvua kubwa vinavyoweza kusababisha mafuriko.

Wataalamu wanasema, El-Nino kwa kawaida huthibitishwa wakati ambapo halijoto ya uso wa bahari katika eneo la tropiki ya Pasifiki ya mashariki inapopanda hadi angalau 0.5C juu ya wastani wa kawaida na kwa muda mrefu na hutokea kila baada ya miaka mitatu au minane na hudumu kwa miezi 9-12.

Mvua bado zinaendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini na Mamalaka ya hali ya Hewa – TMA, ilitangaza uwepo wa mvua za El nino katika Mikoa 14 kwa uwezekano wa kunyesha kwa asilimia 60 ikiwemo Mkoa wa Pwani, Tanga, Geita, Arusha, Kilimanjaro, Mara, Manyara, Simiyu, Kagera, Morogoro, Shinyanga, Kigoma, Mwanza na Dar es Salaam.

Sababu kuu ya mvua hizi mbali na kwamba ni msimu wake umewadia lakini pia madhara makubwa yanachangiwa na mabadiliko ya Tabianchi ambayo yamekuwa yakileta adha mbalimbali ikiwemo mafuriko, dhoruba, ukame na moto wa nyikani, ikichochewa na shughuli za kibinadamu.

Baada ya kukumbwa na ukame ambao haujawahi kushuhudiwa kwa baadhi ya maeneo, kwa wiki kadhaa sasa eneo la Afrika Mashariki linakabiliwa na mvua kubwa na mafuriko yanayohusishwa na El Nino, mfano Nchini Somalia, mvua hizo zimesababisha vifo vya mamia ya watu huku wengine zaidi ya milioni moja wakiyahama makazi yao.

Mwezi Mei mwaka huu, mvua kubwa iliyonyesha ilisababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi nchini Rwanda na kusababisha vifo vya takriban watu 130, huku kati ya Oktoba 1997 na Januari 1998, mafuriko makubwa yaliyochochewa na mvua kubwa ya El Nino yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 6,000 katika nchi tano.

Matukio ya magonjwa ya mlipuko, vifo, uharibifu wa nyumba na miundombinu kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi vilitabiriwa kuwepo kuanzia Oktoba hadi Desemba, 2023 ikiwa ni matokea ya mabadiliko ya tabianchi yanayoleta hali tofauti ikiwemo mvua kubwa, ukame, kimbunga, kubadilika kwa misimu na joto kali.

Athari za mabadiliko ya Tabianchi ni pamoja na njaa, magonjwa, uchumi kudorora baada ya shuguliza za uzalishaji kukwama,vifo na watu kuyahama makazi yao na taarifa ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa – FAO, ilieleza uwepo wa mvua hizo nyingi katika nchi za Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika, Mashariki ya mbali na Amerika ya Kati.

Inaarifiwa kuwa tangu mwaka 1900 kumekuwa na angalau matukio 30 ya El Niño duniani huku El nino ya mwaka 1982-1983, 1997-1998 na 2014-2016 ni miongoni mwa matukio yaliyoweka rekodi na kuleta madhara makubwa huku katika miaka ya 2000, matukio ya El Nino yamejitokeza mwaka wa 2002–2003, 2004–2005, 2006–2007, 2009–2010, 2014–2016, 2018–2019, na sasa mwaka 2023.

Athari za El-nino hutofautiana kila inapotokea, lakini ni tukio linalosababisha matukio makubwa mbalimbali ya hali mbaya ya hewa, ikiwa ni pamoja na ukame, mafuriko, vimbunga, na mawimbi ya joto, ambayo yote ni hatari kwa afya ya binadamu na Shirika la afya duniani limezitaka nchi zijiandae na athari za kiafya ikiwemo uhaba wa chakula, utapiamlo, magonjwa yatokanayo na maji kama vile kipindupindu kutokana na uhaba wa maji au mafuriko na miundombinu ya vyoo.

Ingawa athari halisi za matukio ya El-nino haziwezi kutabiriwa kwa usahihi, lakini Ulimwengu umekuwa ukijiandaa kwa athari za tukio hilo kupitia ufuatiliaji endelevu wa utabiri, tathmini za hatari, uimarishaji wa juhudi zinazowezekana za kukabiliana, kujiandaa, kuwa na mipango ya dharura na kuimarisha mifumo ya kukabiliana na magonjwa na athari zingine ziletazwo na El-nino.

Mbali na hatua zinazochukuliwa na Mataifa kupitia Mamlaka zake kwenye kufuatilia tukio hili na kulitolea taarifa mara kwa mara na hatua za kuchukua, Mwananchi wa kawaida ana jukumu la kufanya, ili kujiandaa na kuchukua tahadhari asiathirike na athari zinazoletwa na El-nino.

Hata hivyo, Jamii pia inapaswa kuzingatia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ikiwemo kuzingatia ushauri wa watalaamu ili kupunguza athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa, kutokukaa, kutembea sehemu hatarishi kama kwenye mikondo ya maji na umeme hasa kipindi cha mvua na upepo mkali na kuhama kwenye maeneo ya mabonde.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzi mbalimbali vya Habari na taarifa za kimamlaka.

Simba Queens kurudisha ubingwa Msimbazi
Twaha Kidiku aingia kambini Morogoro