Duniani kuna mambo mengi ambayo wakati mwingine yanaweza yasikushangaze pekee bali yatakuachia maswali lukuki bila majibu, ni hivi ….. Wakati Dkt. William Bass alipokuwa akitafuta namna ya kuchunguza mwili wa mtu baada ya kufa, ilitokea kuanzishwa kwa Shamba la miili ya Watu linalotumika kwa tafiti, miaka 42 iliyopita.

Mwaka 1981, Daktari huyu alimuuliza Mkuu wa Kitivo cha Sayansi cha chuo kikuu cha Tennessee kama anaweza kutumia sehemu ndogo ya chuo hicho kuweka miili ya watu waliokufa kwa ajili ya kuifanyia utafiti na huo ndio ukawa ni mwanzo wa kuanzishwa kwa shamba hilo liitwalo Anthropology Research Facility.

Kituo hicho kiliomba watu wajitolee kukubali miili yao kutumika na kituo hicho pale watakapokuwa wamekufa na baada ya makubaliano hayo watu hao wanapokufa miili yao huchukuliwa na kutupwa katika shamba hilo kwa namna tofauti tofauti kulingana na mahitaji ya utafiti.

Lakini kwanza walianza na miili inayotupwa kwenye maji yasiyo na kina kirefu, kutelekezwa kwenye nyumba au nyuma ya gari, kutupwa sehemu ya wazi na mingine inafukiwa kwenye kaburi fupi tu na utafiti hufanywa siku nne tangu mtu huyo afariki na kwa kutumia sayansi ya wadudu, wataalamu hao wanaweza kugundua kwa usahihi siku mtu huyo alipofariki kutokana na aina ya funza watakaokutwa katika mwili huo.

Wataalamu wanabainisha kuwa, mtu anapokufa kwa kawaida mwili wake hushambuliwa na funza. Wale funza wa awali wanaposhambulia mwili huo pia huutayarisha kwa ujio wa funza wengine na hutofautiana kwa muda maalum, kutoka aina moja kwenda nyingine na hapo ndipo wanasayansi hao kwa kutumia aina ya funza na wadudu wengine waliowakuta katika mwili huo kupata usahihi.

Hapo Wataalam hugundua namna mtu huyo alivyokufa, kipindi gani alifariki au mwili wake ulitelekezwa mahali hapo wakati gani, lakini pamoja na utafiti wa wadudu, pia mazingira ya eneo husika na hali ya hewa ya tukio kijiografia kulingana na msimu, kwa mfano msimu wa baridi, joto nk, huzingatiwa ili kufanikisha utafiti huo.

Kupitia shamba hilo la miili ya watu, wataalamu wa kisayansi wa kutatua sababu ya vifo visivyo vya kawaida wamefanikiwa sana kufanya tafiti mbalimbali ambazo zimetumika kutatua kesi nyingi za mauaji nchini Marekani. Kupitia utafiti huo hivi sasa, bila kujali mtu amekufa lini, mwili wa mtu unaweza kutoa majibu sahihi sawa sawa na mwili wa mtu aliyekufa hivi punde.

Inaarifiwa kuwa, zaidi ya watu 300 walijitolea miili yao ili kusaidia kituo hicho kufanya utafiti na inaelezwa kwamba zaidi ya miili 120 hupokelewa na kituo hicho kila mwaka. Kutokana na mafanikio ya kituo hicho, kuna vituo vingine vilianzishwa kwa lengo hilo la kutatua vifo visivyo vya kawaida na kesi za mauaji nchini humo.

Vituo hivyo ni pamoja na Texas University kilichopo San Marcos, Western Carolina University kilichopo Cullowhee (ambacho pia hutumika kwa ajili ya mafunzo kwa mbwa wa kunusa), Sam Houston University kilichopo Huntsville na Southwestern Pennsyvania (ambacho kinatumiwa na watafiti wa Chuo kikuu cha Carolina huko Pennsylvania).

Utunzaji Mazingira: Wanawake 200 wakabidhiwa Majiko ya Gesi
Risasi zarindima usiku kucha jirani na Ikulu