Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi amesema kujiamini kwao na ubora wa wachezaji wa Al Ahly ndio kumechangia washindwe kupata ushindi kwenye mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi D, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam juzi Jumamosi (Desemba 02), Young Africans ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na mabingwa hao watetezi wa taji hilo.

Kocha huyo kutoka nchini Argentina amesema kipindi cha kwanza vijana wake walicheza vizuri na kuongoza kwa kila kitu lakini walijawa na haraka hasa walipofika eneo la mwisho la umaliziaji lakini kipindi cha pili walikichukua wapinzani wao Al Ahly na kuwapa wakati mgumu.

“Naweza kusema kabla ya mchezo tulijiamini sana na kutajikuta tunashindwa kutelekeza mambo yetu ya msingi ndani ya uwanja kitu ambacho kilituweka katika wakati mgumu hasa kipindi cha pili baada ya wapinzani kuuchukua mchezo na kututangulia kwa bao la kuongoza.”

“Lakini nawapongeza wachezaji wangu hawakukata tamaa walipambana na kusawazisha bao hilo ambalo ukweli liliturudisha mchezoni ingawa muda tayari ulishakwenda,” amesema Gamondi.

Kocha huyo amesema matokeo hayo siyo mazuri kwao na hakuna aliyeyategemea sababu lengo lao ilikuwa ni pointi tatu, lakini wanayapokea na wanajipanga kuhakikisha wanarekebisha makosa yao na kushinda mechi zijazo kwani uwezo wa kufanya hivyo wanao na nafasi ya kwenda Robo Fainali ipo kubwa kwao.

Rais TFF apongezwa kwa utendaji
Serikali yaipa kipaumbele mifumo ya tahadhari