Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewataka Wananchi kulinda miundombinu ya umeme Vijijini, ili iendelee kuwa na thamani kwa sasa na vizazi vijavyo.
Wito huo ameutoa wkatika Kata ya Makuyuni iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Vijijini Mkoani Tanga, wakati akikagua Mradi wa Kupeleka Umeme awamu ya tatu, mzungungo wa pili.
Amesema, “lindeni miundombinu ya miradi hii kwani ni ya thamani kubwa, tuoneshe ushirikiano kwenye utekelezaji wa miradi hiyo kwani miradi hii haina fidia na inagharamiwa kwa fedha nyingi, ikiwa na lengo la kupeleka huduma kwa wananchi hivyo niwaombe kutoa ushirikiano ili miradi isichelewe.”
Aidha, Kapinga pia amebainisha kuwa, Serikali itaendelea kuleta fedha katika jimbo hilo la Korogwe vijijini na itazidi kusimamia miradi hiyo ikamilike kwa wakati ili wananchi wote wapate huduma ya umeme na kwamba itaendelea kusimamia kwa karibu wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini ili ikamilike kwa wakati.
Kwa upande wake Msimamizi wa miradi ya REA Mkoa wa Tanga Mhandisi Balisidya Myula amesema Jimbo la Korogwe Vijijini lina Jumla ya Kata 29, Vijiji 118 na Vitongoji 610 ambapo vijiji 91 sawa na asilimia 77% vilipatiwa huduma ya umeme kupitia Miradi ya REA III (Mzunguko wa Kwanza na wa Pili) hivyo vijiji 27 ambavyo havina umeme vinataraji kuunganishwa na huduma hiyo kabla ya Juni, 2024.
REA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali kusambaza nishati ya umeme vijijini ambapo Wakala umeendelea kutekeleza Miradi hiyo katika Jimbo la Korogwe vijijini, ikiwa na lengo la kuwapa wananchi huduma ya nishati ili kuboresha huduma za kiafya, elimu na kijamii, sambamba na maendeleo ya kiuchumi.