Ukimya si mzuri hasa pale Wanandoa au wapenzi wanapotofautiana, lakini wapo baadhi ya Wanawake pale inapotokea wametofautiana na wenza wao, hutarajia kuwaona wakipandwa na hasira na kuonyesha hisia zao.
Kitendo cha Mwanaume kuongea kwa hasira na kuonyesha kuchukizwa na jambo fulani, Mwanamke huamini kwamba ni hasira za muda tu na baada ya hapo yatakwisha na maisha yataendelea.
Lakini pale inapotokea kuna jambo ambalo linaonekana limemkera Mwanaume na akakaa kimya bila kusema neno au inawezekana Mwanamke kafanya kosa ambalo anaamini mumewe akijua kutazuka balaa na ikatokea akajua lakini akabaki kimya, jambo hilo linaweza kumnyima raha Mwanamke.
Inawezekana pia Mwanaume akawa amekosea au kuna jambo amefanya ambalo halijampendeza mwenzi wake, lakini pale mke anapokuja juu, Mwanaume akabaki kimya bila kuomba radhi wala kusema neno, jambo hilo pia linaweza kuwa tatizo.
Hakuna mwanandoa anayependa ukimya wa aina hii, kwani kitakachokwenda kichwani mwa mtendewa ni kuhisi amedharauliwa kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo, wakati mwingine kukaa kimya ni jambo jema kwani kuna wakati inaweza kuonekana mwanandoa anayekaa kimya pale anapoudhiwa na mwenzi wake ni utoto na ni njia dhaifu ya kutatua migogoro katika mahusiano.
Lakini kukaa kimya husaidia kuzuia mzozo kuwa mkubwa kwani kutofautiana nakutupiana maneno kwa wanandoa kunachukuliwa kama vita ya kuviziana ambayo mwishowe inaweza kusababisha kuzuka ugomvi na wanandoa kushikana.
Kumbuka kwamba inapotokea kutupiana maneno kwa wanandoa, kuna uwezekano mkubwa wa kila mmoja kutumia fursa hiyo kueleza udhaifu wa mwenzie kwa sababu ya kutawaliwa na hasira kupita kiasi.
Jambo hilo linaweza kuzusha ugomvi mkubwa sana kwa wanandoa lakini kama unataka kuepusha shari, basi ni vyema ukafunga mdomo wako na kukaa kimya japo kwa muda mfupi, hiyo itasaidia sana kuleta amani kwa wapendanao.