Desemba 9 mwaka 1961, yalifanyika mambo makubwa mawili kama sehemu ya maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika ambayo ni kushusha Bendera ya Mkoloni na kupandisha ile ya Taifa huru na wakati huohuo, kupandisha Mwenge wa Uhuru kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Tukio la kupandisha Bendera lilifanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, uliojengwa maalum kwa ajili ya sherehe za uhuru na umuhimu wake, ulikuwa kuonesha kuondoka kwa mkoloni na kwamba kuanzia wakati huo – Watanganyika watakuwa huru kufanya mambo yao wenyewe kwa mustakabali wao.
Kushushwa kwa bendera ile, kulikuwa ni tukio kubwa kwa waliolishuhudia. Kuna wazee wa zamani wanazungumza kuhusu vilio vya furaha vilivyosikika wakati wa tukio hilo lililofanyika saa sita usiku.
Hata hivyo, kule Kilimanjaro, tukio hilo halikujulikana maana yake sana hadi pale Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipozungumza maneno yafuatayo kuhusu tukio hilo, “Tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau.”
Sasa Taifa letu linatimiza Miaka 62 baada ya Uhuru wa Tanganyika – sasa ikifahamika zaidi kwa jina la Tanzania kutokana na Muungano wake na Zanzibar mwaka 1964, ni wakati muafaka wa kutafakari na kuona kama Taifa hili lipo pahali ambapo wale waliopigania Uhuru walitaka iwe wakati huu.