Wagombea watano wa urais wa upinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC, wamesema watafanya maandamano Desemba 27, 2023 jijini Kinshasa, kupinga ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi mkuu wa nchini humo uliofanyika Desemba.
Kwa mujibu wa Jean-Marc Kabunda ambaye ni mwakilishi wa mgombea Martin Fayulu, amesema wanasiasa hao wamewasilisha barua kwa Gavana wa jiji la Kinshasa hapo jana Desemba 23, 2023 wakimuarifu juu ya azma yao hiyo ya kuandamana.
Amesema barua hiyo mbali na kuelezea azma ya maandamano hayo pia inapinga ukiukwaji uliojitokeza wakati na kabla ya zoezi la kupiga kura na uongezwaji wa zoezi la kupiga kura kwa siku moja zaidi.
Hatua hiyo inajiri wakati ambapo Tume ya uchaguzi ya DRC – CENI, ikikiri kuchelewa kuanza shughuli za kupiga kura Desemba 20, kutokana na baadhi ya vituo kuchelewa kufunguliwa huku ikikanusha madai ya kufanyika udanganyifu katika muda ulioongezwa wa upigaji wa kura.