Johansen Buberwa – Kagera 

Watumishi saba wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera, wanashikiliwa na Polisi kwa ajili ya uchunguzi akiwemo Afisa elimu Msingi, kwa kushindwa kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa vya Shule nne za msingi, huku fedha za ujenzi huo zikiwa hazijulikani zilipo.

Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera, Dkt. Abel Nyamahanga ameyasema hayo wakati wa kikao kilichohusisha watumishi wote wa Halmashauri hiyo cha kufunga mwaka na kuzitaja shule za msingi ambazo hazikukamilika kuwa ni Kanyamika, Burigi, Kanyabwenda na Rugasha.

Amesema, watumishi wengine wanaoshikiliwa mbali na afisa Elimu Msingi ni Wahandisi wa ujenzi watano na Afisa manunuzi mmoja ambao walisimamia ujenzi wa vyumba vya madarasa chini ya kiwango na kushindwa kukamilika kwa wakati huku fedha zikiwa zimetumika zote zilizotengwa na mafundi bado wanaendelea kudai fedha zao kwa Halmashari hiyo.

“Napiga marufuku kutumia mapato ya ndani kinyume na utaratibu kwenye ukamilishaji wa miradi ambayo imeshindwa kukamilika kutokana na usimamizi hafifu kwa watumishi kwani tayari imeshatengewa fedha ili ikamilishe miradi hiyo yote amesema Dkt. Nyamahanga.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Christina Akio amesema atahakikisha anasimamia utendaji kazi wa watumishi, ili miradi yote inayokuwa imeanzishwa ikalimilike kwa wakati na ubora.

baadhi ya watumishi waliozungumza na Dar24 Media akiwemo Evart Kagaruki na Charles Ntaki wamesema watahakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano, ili kuwahudumia wananchi kwa weledi na kuondoa changamoto zilizopo ambazo zinasababisha kuyumba kwa utendaji kazi ikiwemo kushindwa kukamilika kwa baadhi ya miradi ya maendeleo.

Oparesheni Dawa za Kulevya: Hakuna atakayeonewa - Chalamila
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Desemba 29, 2023