Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Adel Amrouche amesema ataendelea kutumia mechi za kirafiki kuhakikisha anapata kikosi imara kitakachokwenda kwenye Fainali za Mataifa ya Africa ‘AFCON 2023’ zitakazofanyika Ivory Coast kuanzia Januari 13 hadi Februari 11 mwaka huu.
Amrouche amesema hayo baada ya kushuhudia mchezo wa Kirafiki kati ya timu ya soka ya Tanzania Bara “Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes uliochezwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar juzi Jumatano (Desemba 27) na kumalizika kwa suluhu.
Amesema mchezo huo ulikuwa wa kimbinu zaidi na timu zote zilicheza kwa kutegeana lakini ulikuwa mchezo mzuri japo timu zote zilishindwa kutumia nafasi kadhaa walizopata.
“Ulikuwa mchezo mzuri na waliokuwa nje walipata nafasi ya kucheza na kuonesha kile walichonacho. Bado tupo kwenye kupata wachezaji 27 kutoka 55 ambao wapo kambini,” amesema.
Amesema bado wana mechi nyingine za kirafiki mbele, hivyo ataendelea kufanyia kazi upungufu na mpaka wakati wa mashindano atakuwa na kikosi kizuri na imara.
Baada ya mchezo huo, Taifa Stars imeendelea na kambi Zanzibar na keshokutwa Jumapili (Desemba 31) itakwenda kuweka kambi Misri ambako itacheza mchezo wa kirafiki na mabingwa hao wa kihistoria wa AFCON.
Mido Mnigeria aibukia Tabora United
Taifa Stars ambayo inashiriki mashindano ya 34 ya AFCON mchezo wa kwanza watacheza Januari 17 dhidi ya Morocco, mchezo wa pili Januari 21 dhidi ya Zambia na mchezo wa tatu Januari 24 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC).
Hii ni mara ya tatu Tanzania inashiriki fainali za AFCON ambazo zitafanyika katika miji mitano ya Abidjan, Yamoussoukro, Bouake, Khorogo na San Pedro.