Serikali imemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Adolf Nduguru kuwabadilisha wataalamu wa mifumo wa idara ya uhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma kwa sababu za uwajibikaji.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Deogratius Ndejembi wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa Shule ya Wasichana ya Mkoa wa Kigoma inayojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.
Amesema, hatua ya kuwabadilisha wataalamu hao wa mifumo inatokana na uwepo wa changamoto iliyojitokeza katika idara ya uhasibu na fedha iliyoshindwa kusimamia na kutatua tatizo la mifumo iliyopo ndani ya Halmashauri.
Aidha, Ndejembi pia amemtaka Kaimu Mhandisi wa Halmashauri hiyo, Philipo Marco kuhakikisha anasimamia ipasavyo ujenzi huo, ili ukamilike kwa wakati.