Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssoupha Dabo, amesema kuwa maandalizi ya mchezo wa Robo Fainali dhidi ya Singida Fountain Gate, yamekamilika na wako tayari kwa ajili ya mechi hiyo.

Azam FC wanashuka kuwakabili Singida Fountain Gate wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa mabao 4-1 kwenye mashindano ya Mapinduzi ya mwaka 2023.

Akizungumza, kocha Dabo amesema maandalizi ya mchezo dhidi ya Singida Fountain Gate yamekamilika vizuri na kikosi kiko tayari, ingawa kuna baadhi ya wachezaji wana majeraha na wengine wamechoka baada ya kutumika sana.

“Licha ya kututoa kwenye Nusu Fainali mwaka jana, lakini kwetu huu sio mchezo wa kisasi, nimewaambia wachezaji wangu wasahau kwa sababu ni kitu kilichopita.

“Kama ni kisasi tulicheza nao Tanga tukashinda 2-0 kwenye Ngao ya Jamii ingawa naamini kwenye mchezo wa leo Jumatatu (Januari 08) watakuja kivingine ili wapate matokeo na sisi tunahitaji kwenda Nusu Fainali,” alisema Dabo.

Amesema mchezo huu ni muhimu kwao kwani malengo yao ni kushinda makombe ya ndani wanayoshiriki ili waweze kutimiza malengo yao.

Justine Ndikumnana aondoka Coastal Union
Mwana FA achekelea maandalizi Taifa Stars