Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana na Klabu ya Young Africans Augustine Okrah, anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa wiki tatu, akiendelea kuuguza majeraha yake.
Nyota huyo alishindwa kuendelea na mchezo wa tatu wa Hatua ya Makundi wa Kombe la Mapinduzi baada ya kugongwa katika mshipa wa pua na beki wa KVZ mchezo uliopigwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Young Africans zinaeleza kuwa kiungo huyo amewekwa chini ya ulinzi wa jopo la madaktari wa timu hiyo huku akiendelea kupata matibabu.
Mtoa taarifa huyo amesema kuwa kiungo huyo anatarajiwa kuanza mazoezi mepesi ya binafsi baada ya majuma matatu kabla ya kujiunga na wenzake.
Ameongeza kuwa kiungo huyo kwa sasa anaendelea na yupo katika matibabu maalum ya madaktari hao, ili kuhakikisha anapona haraka na kurejea uwanjani.
Okrah anaendelea vizuri na afya yake, licha ya kuwepo chini ya uangalizi wa madaktari wetu kuhakikisha anapona haraka na kurejea haraka uwanjani.
“Okrah alipata majeraha makubwa ambayo madaktari wetu walijitahidi kupambana kuhakikisha anapata nafuu, matibabu ambayo amepangiwa na madaktari wetu ni ndani ya wiki tatu atakuwa amepona kabisa,” amesema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia hilo Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi amesema kuwa: “Okrah anaendelea vizuri hivi sasa, lakini ataanza kuonekana uwanjani baada ya wiki tatu, hatuoni sababu ya kumuwahisha mapema, kwani wapo wachezaji wengi katika kikosi chetu.”