Kiungo Mkabaji wa Mali, Yves Bissouma anatazamia kuiwakilisha nchi aliyozaliwa kwenye fainali za mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’, zinazoendelea nchini Ivory Coast.
Bissouma, anayecheza soka kulipwa England na klabu ya Tottenham Hotspur alikuwa akizungumza na CAFOnline akitokea kwenye kambi ya timu ya Mali, Korhogo ambapo timu hiyo inajiandaa kuikabili Afrika Kusini, Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly.
“Haya yatakuwa mashindano maalumu kwangu kwa sababu nilizaliwa hapa. Ni kama hazina na mimi kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika kwenye nchi niliyozaliwa ni kitu cha kipekee. Natumairi kufanya hivyo na wenzangu na kuwafanya mashabiki wetu wajivunie,” alisema Bissouma.
Mali waliwasili kwenye mji wa Korhogo, ljumaa (Janauri 12) na wako Kundi E na timu za Afrika Kusini, Tunisia na Namibia.
“Tuko kwenye kundi la kuvutia ambalo linahitaji hadhari kubwa. Hatuchukuli kitu chochote poa na tutafanya kila linalowezekana kwenye mashindano haya.” alisema kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27.
Mali itacheza mchezo wake wa kwanza wa mashindano hayo dhidi ya Afrika Kusini, mchezo ambao ni kama kisasi cha mwaka 2013 wakati timu hiyo kutoka Afrika Magharibi walipoiondosha kwenye hatua ya Robo Fainali Afrika Kusini.