Johansen Buberwa – Kagera.

Jeshi la Polisi Mkoani Kagera, linawashikilia watu wawili, Gaudiozi Yepa (42), mfanyabiashara na Philemoni Reveliani (39), Mvuvi wa kisiwa cha Msira, kwa tuhuma za ubakaji wa Watoto.

Akizungumza na Vyombo vya Habari, Kamanda Polisi Mkoa wa Kagera Kamishina Msaidizi wa Polisi, Blasius Chatanda amesema mtuhumiwa wa kwanza (Yepa), alitenda kosa hilo Januari 2, 2024 mtaa wa Bomani, uliopo Kata ya Kayanga Tarafa ya Bugene Wilayani Karagwe.

Amesema, Yepa alimrubuni mtoto huyo (10), ambaye ni Mwanafunzi wa darasa la nne kwa kumwambia apande gari lake lenye namba za usajili T 639 BKP aina ya Peugeot ili ampeleke nyumbani kwao na baada ya mtoto huyo kupanda ndipo alimbaka kwa nguvu na kumsababishia maumivu mwilini.

Kamanda Chatanda amesema, kosa la mtuhumiwa wa pili (Reveliani), ambaye ni baba wa kambo wa mtoto (5), anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 26, 2023 Tarafa ya Rwamishenye Manispaa ya Bukoba, baada mama wa mtoto huyo Gaudensia Charles (30), kwenda kituo cha Afya.

Amesema kwa sasa hali za Kiafya kwa watoto hao zinaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Nyakahanga Wilayani Karagwe na Hospitali ya Rufaa Mkoa Kagera na kudai kuwa watuhumiwa watafikishwa Mahakamani mara baada ya Upelelezi na taratibu za kisheria kukamilika.

Aidha, Kamanda Chatanda amesema jeshi hilo linatoa onyo kwa watu wote wenye tabia za kwenda kinyume na maadili kuacha mara moja na halitasita kuwachukulia hatua za kisheria huku likiwaomba wananchi kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha Mkoa wa Kagera unakuwa Salama.

Yves Bissouma: AFCON 2013 ni maalum kwangu
Mazingira bora uwekezaji yaivutia AngloGold Ashanti kuwekeza Nchini