Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha ameanza mapumziko mafupi akiwa kwao Algeria, lakini amewatumia salamu mastaa wa timu hiyo kwamba watakuwa na kazi nzito ili kupambana na timu mbili za juu.
Benchikha amesema usajili walioufanya una deni la kwenda kuthibitisha kwa kuirudisha Simba SC kwenye mbio za ubingwa, kwa kuzishusha Azam FC na Young Africans ambazo zipo juu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Kocha huyo amesema, Simba SC haitakiwi kuendelea kukaa chini ya timu hizo kubwa mbili na mara baada ya wachezaji kurejea kutoka mapumziko mafupi wanatakiwa kufanya maandalizi mazito.
Simba SC itarudi kambini Januari 25 baada ya kocha huyo kutoa mapumziko mafupi kwa wachezaji wote kurudi makwao kisha kurejea tena kazini haraka.
“Nimewaambia hakuna mchezaji anayetakiwa kukosa siku ya kwanza ya mazoezi bila sababu ni bora uwahi kuliko kuchelewa tunatakiwa kuanza kazi ngumu kwa pamoja,” amesema Benchikha na kuongeza;
Tumewaongeza wachezaji wapya kila mmoja ndani ya timu sasa ana hamu ya kuona malengo ya klabu yanafikiwa, nani wa kukamilisha hilo? Ni sisi kwenye timu tuna kazi ngumu lakini inawezekana kama kila mmoja atajitoa kwa asilimia mia moja.
“Simba SC haitakiwi kuendelea kuwa chini kwenye msimamo tunatakiwa kuwa juu na hili halitawezekana kama tutaendelea kufanya kazi kwa mazingira ya kawaida, tunatakiwa kufanya kazi kwa malengo na kuweka juhudi.”
Kwenye msimamo wa ligi, Simba SC ipo nafasi ya tatu ikiwa alama 23, Young Africans ina alama 30 na Azam inayoongoza msimamo ikiwa na alama 31 licha ya kutofautiana mechi ilizocheza, Azam ikicheza 13, Simba 10 na Young Africans 11.