Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini, Jenerali Jacob Mkunda ametembelea Mradi wa Ujenzi wa Nyumba 5,000 Msomera Wilayani Handeni Mkoani Tanga, unaotekelezwa na Jeshi la Kujenga Taifa, kwaajili ya Wananchi wanaohamia kwa hiari yao kutoka Hifadhi ya Taifa Ngorongoro.
Akizungumza katika ziara hiyo hii leo Januari 20, 2023 Jenerali Mkunda amesema maendeleo ya mradi ni mazuri, kutokana na ushirikian kati ya taasisi mbalimbali za kisekta.
Amesema,“nimepita na nimejionea mwenyewe na kiujumla maendeleo ya mradi ni makubwa sana kwasababu kuna mashirikiano makubwa na mazuri ya taasisi mbalimbali ya kisekta, Vijana wetu wamepewa kazi yao na inakwenda vizuri na nimeridhishwa sana na utendaji wao wa kazi.”
Jenerali Mkunda pia amewapongeza vijana hao kwa kuendelea kufanya kazi kwa moyo na uzalendo kwani wanatekeleza jukumu lao la msingi la Jeshi la Wananchi wa Tanzania kupitia SUMA JKT ambayo ni majukumu ya kawaida.
“Mimi natambua na wao wanatambua hilo na ndiyo maana wanafanya kazi hii kwa moyo na kwa nguvu kubwa ya kizalendo, hivyo waendelee kufanya kazi ya kizalendo kwa kuwatumikia Watanzania, Wananchi wenzetu”. Amesema Jenerali Mkunda
Itakumbukwa kuwa Serikali kupitia wizara ya mali asili na utalii chini ya mamlaka ya hifadhi ya ngorongoro iliingia makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba 5000 na shirika la uzalishaji mali la SUMA JKT katika maeneo ya Msomero Wilayani Handeni, Kijiji cha Saunyi Wilaya ya kilindi pamoja na Wilayani Simanjiro.