Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema hali uzalishaji wa sukari katika viwanda saba nchini imeshuka hadi kufikia tani 1,000 kwa siku kutokana na mvua za El-nino zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini, ambazo zimeathiri hali ya uvunaji wa miwa mashambani na kupunguza kiwango cha sukari katika miwa kwa zaidi ya asilimia 25.

Akitoa kauli ya sserikalihii leo Januari 20, 2024 kuhusu hali ya sukari nchini, Bashe amesema katika kukabiliana na uhaba wa sukari ambao sasa umefikia tani 30,000, serikali imetoa kibali kwa wenye viwanda kuagiza sukari tani 100,000 ambayo inatarajiwa kuwasili nchini tarehe 23 – 24 Januari mwaka huu.

Amesema mahitaji ya sukari kwa siku nchini ni tani 1,500 na kutokana na hali hiyo bei ya sukari imepanda kutoka 2,700, 3000 hadi kufikia 4000 na kwamba uhaba wa sukari sasa umefikia tani 30,000 ikilinganishwa na uhaba wa tani 200,000-150,000 kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

“Uzalishaji wa sukari katika taifa kwa kipindi cha miaka mitatu uliendelea kuongezeka kiasi kwamba sugar gap kwa mwaka jana ilishuka mpaka kufika wastani wa tani 30,000 na mwaka huu tulitarajia kumaliza kabisa gap ya sukari katika Taifa letu,” alisema.

Aidha Bashe ameongeza kuwa, “kufikia kipindi cha msimu wa Aprili mwaka huu tungeweza kufikia uzalishaji wa tani zaidi ya 500,000. Mwaka jana tulizalisha tani 460,000 tukawa na gap ya tani 30,000 ambazo tuliagiza na tulijua kwamba tunafika mahali pa kujitosheleza.”

“Kwa kipindi cha miaka mitatu Sugar gap yetu imeshuka kwa wastani wa tani 150,000- 200,000 mpaka kufika tani 30,000. Hizi ni kazi kubwa ambazo zimefanywa na sekta binafsi kwa kushirikiana na serikali,” amesema.

Amesema mwaka huu wamepata ‘shock’ kutokana na uzalishaji wa viwandani kushuka na hata hivyo kutokana na hatua zilizochukuliwa anaamini ifikapo katikati ya Februari hali ya upatikanaji wa sukari itaanza kurejea katika hali ya kawaida na kutokuwa na madhara yoyote.

“Tunaamini kwamba mvua hizi zitaendelea mpaka mwezi wa Februari na Machi, tutaendelea kutoa idhini ya uagizaji wa sukari ili kuendelea kumlinda mlaji na tumeagiza bodi ya sukari kufanya kazi kwa karibu na wenye viwanda kuhakikisha stability na bei ya sukari inarudi katika hali yake,” amesema.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Januari 21, 2024
Jenerali Mkunda akubali kasi Ujenzi Nyumba 5,000 Msomera