Imefahamika kuwa Klabu ya Simba SC inaendelea na mpango mkakati wa ndaaani ambao lengo lake ni kurejesha hadhi ya timu hiyo katika michuano ya ndani ya ila ya Kimataifa.
Hii ina maana ya kwamba uongozi wa Klabu hiyo ya Msimbazi umedhamiria kupitisha fagio kwa mastaa wasumbufu ndani ya kikosi chao.
Taarifa kutoka ndani ya Uongozi wa Klabu ya Simba SC zinasema wamebaki watu wawili ama watatu, ili kufanikisha dhana ya kusafisha udhaifu ambao huenda umekuwa tatizo ndani ya kikosi cha Mnyama, ambapo staili kama hiyo ya Simba SC iliwahi kufanywa na Young Africans miaka michache iliyopita.
Habari zinaeleza kuwa Uongozi wa Simba SC umefanya uchunguzi na kuona kuna kikundi cha mastaa watatu ambapo kama wakikimaliza, basi makocha na timu nzima itafanya kazi kwa sauti na kwa nguvu moja kama ilivyo kauli mbiu yao.
Mastaa hao ambao wanaipasua kichwa Simba SC ni Clatous Chama ambaye kwa sasa yupo nje ya kikosi baada ya kusimamishwa akidaiwa kukwaruzana na mmoja wa makocha wa timu hiyo.
Wengine ni mshambuliaji Moses Phiri ambaye tayari imeshamuondoa na kumpeleka kwa mkopo Power Dynamos ya Zambia na yule wa tatu ni Luis Miquissone.
Mastaa hao watatu, Simba SC inataka kuwaondoa wawili kati yao ili kuvunja umoja wao wa ndani ya kikosi ambao umekuwa ukitajwa kuwa mgumu kufanya mambo yaende kwa wepesi.
Simba SC ilibakiza hatua chache tu kumtena Chama kwenye dirisha dogo la usajili ikitajwa kuwa ndio mwendelezo wa hesabu hizo, lakini ikakosa mtu sahihi wa kuziba nafasi yake ndani ya kikosi hicho.
“Yule Tchakei (Marouf) tungempata tungeachana na Chama. Imekuwa shida kidogo kuwa na hawa watatu.
Miquissone hana shida sana, lakini tunaona kama anapokuwa na Chama na Phiri asingeweza kufanya kazi vizuri,” kilieleza chanzo chetu ndani ya Simba.
Za ndaaani kabisa zinasema kwamba, Simba SC inaona baada ya kusimamishwa kwa Chama, Miquissone ameanza kurejea kwenye ubora wake akijituma kwa nguvu ndani ya kikosi hicho.
Hesabu kubwa kwa sasa ni kuachana na Chama ambapo mabosi wa klabu hiyo wapo kwenye msako mkali wa kumsaka mrithi wake.
YANGA ILIPITA HUMO HUMO
Kama itakumbukwa vyema Young Africans ilipita katika njia hiyohiyo mara mbili wakati inajenga kikosi chake bora ilicho nacho ambacho kilichukua mataji yote kwa misimu miwili mfululizo.
Mapema Young Africans iliwatema kwa mpigo waliokuwa mabeki wa klabu hiyo, Juma Abdul na Kelvin Yondani pamoja na kiungo Haruna Niyonzima kwa kugoma kuwaongezea mikataba ili kuondoa kundi lao.
Baada ya kuwaondoa kwa akili wakongwe hao mabosi wa Young Africans waliingiza damu mpya ambapo ilikuwa rahisi kwa makocha wa timu hiyo kudili nazo kwa nidhamu.
Msimu uliopita Young Africans pia iliendeleza hesabu hizo ikimtema winga wake Bernard Morrison kwa kugoma kumuongezea mkataba baada ya kudaiwa kuwa raia huyo wa Ghana ndiye anaondoa utulivu kwa kiungo mshambuliaji, Stephanie Aziz KI.
Baada ya kumuondoa Morrison, Azizi KI alitulia na haraka msimu huu raia huyo wa Burkina Faso aliuanza kwa kishindo akiwa na moto wa kufunga mabao na ndiye kinara wa mabao ndani ya kikosi hicho na hata Ligi Kuu Bara akifunga mabao 10.