Rais wa Klabu ya Young Africans, Hersi Said amesema wapo tayari kumuuza kinara wa mabao wa timu hiyo, Stephane Aziz Ki endapo kuna timu yoyote itamuhitaji.
Kinara huyo wa mabao kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ameonesha kiwango bora kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zinazoendelea nchini Ivory Coast akiwa na timu yake ya taifa ya Burkina Faso kiasi cha kuzivutia timu nyingi za Ulaya na Afrika.
Akizungumza mjini Dodoma ambako klabu hiyo ilikuwa na kikao cha kwanza cha kikatiba, Rais huyo amesema hawawezi kumzuia mchezaji endapo atahitajika na timu yoyote sababu mpira ni biashara.
“Hatuwezi kumzuia asiondoke kama kuna timu yoyote inahitaji huduma yake waje mezani, unajua mpira ni biashara tukimuuza tutapata pesa na kwenda sokoni kununua mchezaji mwingine,” amesema Hersi.
Rais huyo amesema kumngang’ania mchezaji kuna madhara yake ikiwemo kuwepo kwa migomo na hujuma na Young Africans ni klabu inayotoa fursa kwa vijana ndio maana walimuuza Fiston Mayele akiwa kwenye kiwango cha hali ya juu.
Amesema mbali na Mayele, hata wao waliuziwa Aziz Ki baada ya kuvutiwa naye na klabu yake ilikubali hivyo haoni sababu ya kumzuia ilimradi taratibu zifuatwe na biashara ifanyike.
Inaelezwa baadhi ya mawakala waliopo Ivory Coast wamekuwa wakimsumbua Aziz Ki, wakitaka kumtafutia timu Ulaya baada ya kuvutiwa na kiwango chake.