Bertina Mangosongo.

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2016/2017 hadi Desemba 2023, imewalipa wazabuni na wakandarasi wa ndani zaidi ya shilingi trilioni 2.1 kati ya madai ya zaidi ya shilingi trilioni 3.1 yaliyowasilishwa.

Dkt. Nchemba ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, aliyetaka kufahamu kiasi cha fedha ambacho Serikali imewalipa ama kukataa kuwalipa wazabuni na wakandarasi wa ndani baada ya kuwasilisha madai yao na kufanyiwa uhakiki.

Amesema, “jumla ya madeni ya wazabuni na wakandarasi yaliyowasilishwa kwa uhakiki yalikuwa zaidi ya sh. bilioni 3,110.33, kati ya kiasi hicho madeni yaliyolipwa ni zaidi ya sh. bilioni 2,128.54 ambapo sh. bilioni 1,032.13 ni madeni ya wazabuni na sh. bilioni 1,096.41 ni madeni ya wakandarasi.”

Mwigulu ameongeza kuwa, madeni ya shilingi bilioni 981.79 yalikataliwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kukosekana kwa nyaraka, madeni kubainika kulipwa tayari, pamoja na makosa ya ukokotoaji.

Ameongeza kuwa, Serikali kwa kutambua umuhimu na mchango wa Sekta Binafsi katika maendeleo na uchumi wa Taifa, imeendelea kutenga na kulipa madeni ya wazabuni na wakandarasi yaliyohakikiwa na kukubaliwa.

“Serikali imeongeza bajeti ya kulipa madeni kutoka wastani wa shilingi bilioni 400 hadi shilingi bilioni 700 kwa mwaka na kuahidi kuwa madai ya wazabuni na wakandarasi yataendelea kulipwa kadri watakavyowasilisha hati zao za kukamilisha kazi,” alisema.

Hersi Said: Tutamuuza Stephane Aziz Ki
Akamatwa na fuvu la binadamu, vipande vutatu vya ngozi