Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa – SUKI na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM – MCC, Rabia Abdallah Hamid amesema CCM itaongea na taasisi za benki ambazo ziLIwakopesha Wafanyabiashara wa soko maarufu la Mbuyuni lililopo Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, lililoungua kwa moto na kupelekea biashara za Wafanyabiashara zaidi ya 2,500 kuteketea.
Moto huo, unadaiwa kuanza kuwaka majira ya saa sita usiku wa kuamkia leo Februari 6, 2024 huku chanzo chake kikiwa bado hakijajulikana, na kusababisha hasara kubwa kwa Wafanyabiashara hao ambao asilimia kubwa wamedai walikuwa wakijiendesha kwa mikopo.
Amesema, Viongozi wanapaswa kuanza kutambua idadi ya Wafanyabiashara waliokuwa na mikopo na ambao walikuwa na utaratibu wa kurejesha marejesho kila mwezi, ili kuona namna ya kuwasaidia kwa utaratibu watakaoutoa.
“Viongozi mnapaswa muanze mara moja kuwatambua ni wafanyabiashara wangapi ambao walikuwa na mikopo na asiachwe hata mmoja kwani kunautaratibu wa kurejesha marejesho kila mwezi lakini kwenye hili sisi chama cha Mapinduzi tutaenda kukaa na taasisi hizo ili kuhakikisha wafanyabiashara hawa hawanyanyasiki katika kipindi hiki,” alisema Rabia.