Johansen Buberwa, Bukoba – Kagera.
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Bukoba Vijijini Mkoani Kagera, limejipanga kutokomeza alama ya sifuri katika shule ambazo zimekuwa zikifanya vibaya kwenye mitihani ya kitaifa kwa msingi na sekondari kwa kuweka mikakati mipya mwaka huu.
Wakijadili hoja mbalimbali za Madiwani wa kata Katoma, Kanyengereko na Viti Maalumu zilizowasilishwa na Madiwani baada ya kupokea taarifa ya kamati ya Elimu, Afya na Maji kwenye kikao cha Baraza hilo, kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2023/2024 wamesema mpaka sasa kwenye kata zao kuna upungufu mkubwa na uhaba wa walimu.
Wamesema Walimu hao ni wale wa masomo ya Sayansi kwa Shule za Sekondari na Msingi na kwamba waliopo wanazidiwa kwa kuwa na vipindi vingi ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi shuleni, huku wakiiomba Serikali kuongeza bajeti kwa mwaka ujao wa fedha, ili kuweza kutatua jambo hilo na kuongeza ufaulu.
Wakijibu hoja hizo za kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Afisa Elimu Msingi, Devotha Mtesigwa na Maya Mbaraka ambaye ni Afisa Elimu Sekondari, wamesema kwa shule zilizofanya vibaya kwenye mitihani mwaka jana, wameanza na hatua za Walimu kupewa Barua huku wengine wakibadilishiwa madaraka.
Aidha, wamesema kwa Shule zilizofanya vibaya zipo chini ya uangalizi huku shule za Sekondari zikifunga mfumo wa kanzidata na matarajio ya mwaka 2025 Halmashauri hiyo itanunua A zote kwa Walimu wa Shule za Sekondari zitakazofanya vizuri, ili kuongeza motisha pamoja na mpango wa kujenga Shule mpya za kidato cha tano na sita kutumika kama njia ya kuongeza ufaulu.
Hata hivyo, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Jasson Rwankomezi ametoa wito kwa Kamati za Shule, Wenyeviti na Watendaji kutokaa ofisini na badala yake wakashughulie elimu kwenye maeneo yao, ili kukuza ufaulu wa elimu.