Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Serikali imeamua kuendeleza vyanzo vya umeme wa Jotoardhi, vitakavyo ongeza nguvu katika vyanzo vilivyopo vya Maji na Gesi Asilia, ili kuhakikisha nchi inazalisha umeme wa kutosheleza mahitaji ya wananchi wake.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Februari 20, 2024 mara baada ya kukagua vyanzo vya Jotoardhi vya Kiejo-Mbaka (60MW) na Ngozi (MW 70) mkoani Mbeya akifuatana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Juma Homera.
“Miradi hii ya Jotoardhi sasa lazima ianze, tutaanza na megawati 10 hapa Kiejo-Mbaka na Ngozi tutaanza na megawati 30 huku nyingine zikifuata, na hii inajumuisha miradi mingine kama wa Jua wa Kishapu (150 MW) ambao umeanza kutekelezwa, miradi ya umeme wa upepo ukiwemo wa Makambako na mradi wa Malagarasi ambao mkandarasi ameshasaini mkataba tayari kwa kuanza kazi.” Amesema Dkt. Biteko.
Amewaelekeza watendaji wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) kufanya kazi zinazoleta matokeo na si stori kwani Serikali inatafuta fedha za kutekeleza miradi hiyo na wajibu wa watendaji wa Taasisi hiyo ni kuhakikisha miradi hiyo inafanikiwa.
Kuhusu changamoto ya umeme, amesema kuwa, imetokana na vyanzo vya umeme nchini kwa muda mrefu kujikita kwenye makundi matatu tu ambayo ni maji (570MW), Mafuta na Gesi Asilia.
Amesema, kwa sasa, vyanzo vya umeme vinatokana na Gesi Asilia na Maji ambavyo bado havitoshelezi mahitaji kutokana na kuzidi kukua kwa maendeleo, idadi ya watu kuzidi kuongezeka, miji kukua na umeme sasa kuwa ni hitaji muhimu na si anasa.
Ameongeza kuwa, pamoja na kutegemea megawati 235 kutoka mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) na megawati 27 kutoka Rusumo, maboresho ya mitambo mingine ya umeme yanaendelea katika vituo mbalimbali.
Awali, Meneja Mkuu wa TGDC, Mhandisi Mathew Mwangomba, amesema kampuni hiyo ina miradi mitano ya kipaumbele nchini ambayo ni Kiejo-Mbaka, Ngozi, Songwe, Ruhoi na Natron.
Ameeleza kuwa, kwa Mkoa wa Mbeya miradi ya kipaumbele ni Ngozi na Kiejo-Mbaka ambapo mradi wa Ngozi unatarajiwa kuzalisha megawati 70 na Kiejo-Mbaka unatarajiwa kuzalisha megawati 60.
Katika mradi wa Ngozi, amesema kuwa, utatekelezwa kwa awamu huku awamu ya kwanza ikitarajiwa kuzalisha megawati 30 na fedha zimeshapatikana ili kuhakiki rasilimali ya Jotoardhi kwenye eneo hilo.
Kuhusu mradi wa Kiejo-Mbaka, amesema kuwa, unatarajiwa kuzalisha megawati 60 ambapo zitaanza kuzalishwa megawati kumi (10) ambazo utekelezaji wake utagharimu Dola za Marekani milioni 75.64 sawa na shilingi Bilioni 175.88.
Ameongeza kuwa, katika kuhakikisha nishati ya Jotoardhi inapatikana Tanzania, TGDC imechonga visima vifupi vya mita 300 ambavyo viliwezesha kupatikana kwa temperature takriban 75 na hii ikithibitisha kwamba kuendelea kuchimbwa kwa visima hivyo kuanzia mita 1500 hadi 1900 itapatikana temperature ya kutosha kuweza kuzalisha umeme.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amemhakikishia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuwa, Mbeya inamuunga mkono Rais, Dkt. Samia katika kulinda vyanzo vyote ya umeme vinavyogundulika pamoja na utunzaji wa mazingira ambayo yanapelekea vyanzo hivyo kuzalisha umeme kwa ufanisi.