Timu ya taifa ya Wanawake, wenye umri chini ya miaka 20 ‘Tanzanite’ imeanza mazoezi ya utimamu wa mwili, kujiandaa na mashindano Afrika.
Michuano ya Afrika imepangwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Machi 8, mwaka huu jijini Accra, Ghana.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’, Cliford Ndimbo, amesema kuwa, Tanzanite iliyopiga kambi katika Hoteli ya Aura, imeanza mazoezi tangu mwanzoni mwa juma hili jijini Dar es salaam.
Ndimbo amesema baada ya mazoezi ya awali ya utimamu wa mwili kufanyika kwa siku mbili, Tanzanite iliungana na Twiga Stars katika mazoezi ya uwanjani yanayofanyika katika uwanja wa Kituo cha Ufundi cha TFF, kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam.
“Tanzanite na Twiga Stars zinafanya mazoezi pamoja kujiandaa mashindano ya Afrika na Olimpiki dhidi ya Afrika Kusini, kambi inaendelea vizuri chini ya Kocha Mkuu, Bakari Shime,” amesema Ndimbo.
Twiga Stars itaikaribisha Afrika Kusini katika mechi ya awali itakayopigwa keshokutwa Ijumaa (Februari 23) katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.