Maafande wa jesho la Magereza Tanzania ‘Tanzania Prisons’ wametamba wako tayari kuikabili Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa keshokutwa Jumapili (Februari 25) kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini Mbeya, lakini hawataingia ‘kichwa kichwa’ kwa sababu wanajua wapinzani wao wako ‘moto’ kwa sasa.

Kocha Msaidizi wa Tanzania Prisons, Shaban Mtupa, amesema wanaendelea vyema na maandalizi ya kuiwinda Azam FC wakitarajia mchezo huo utakuwa mzuri na mgumu.

Mtupa amesema Azam FC wamefanya usajili mzuri msimu huu na ni moja ya timu yenye mbinu kali uwanjani hivyo lazima wajipange vizuri kuwakabili.

“Tunajua tunacheza na timu kubwa ambayo iko moto kwa sasa na yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa, hivyo tunaendelea kujipanga. Tunaendela kufanyia kazi baadhi ya vitu kwenye uwanja wa mazoezi ili siku ya mechi tuwe vizuri na kupata matokeo, malengo yetu msimu huu ni kumaliza ndani ya nafasi nne za juu ili uzipate nafasi hizo lazima ujitoe hasa, “amesema Mtupa

Naye Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hamad Ally amesema wanaendelea kufanyia kazi mapungufu katika safu ya Ushambuliaji ili kuhakikisha Jumapili wanapata mabao na wanazibakisha pointi tatu nyunbani.

“Marekebisho ninayoendelea kuyafanya naamini yatanipa matokeo mazuri katika mchezo huo ambao utakuwa na upinzani mkubwa,” amesema Ally.

Kocha huyo amesema lengo lake ni kushinda michezo yote ya nyumbani ikiwa pamoja na kushika nafasi za juu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Amesema wachezaji wote wanaendelea vyema kiafya na kudai kwa wale ambao walikuwa majeruhi hali zao zinaendelea kuimarika.

Ameongeza nyota wake, Salum Kimenya na Doto Shabani, ambao walikuwa wamepata majeraha kwa sasa wameanza kufanya mazoezi mepesi mepesi .

Tanzania Prisons katika mechi tano zilizopita imeshinda tatu imetoka sare mechi moja na kupoteza mchezo moja dhidi ya Yanga wakati Azam katika mechi zake tano zilizopita imeshinda tatu na kutoka sare mechi mbili.

Al-Itihad kumng'oa Son Ulaya
Young Africans kuibadilikia CR Belouizdad