Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger amewaonya mabosi wa Liverpool kwamba wasimtumie Jurgen Klopp kama mshauri wa kupendekeza Kocha mpya atakayechukuwa mikoba yake baada ya yeye kuondoka mwisho wa msimu.

Klopp ambaye ataondoka Liverpool mwisho wa msimu huu ikiwa ni baada ya kuhudumu kwa miaka tisa, hivi karibuni alifanya mahojiano na kusema kwamba Xabi Alonso ni mmoja kati ya makocha wanaofaa kuifundisha timu hiyo.

Kocha huyu amekuwa sehemu ya mabadiliko ya Liverpool akihusika kwenye masuala mbali mbali kuanzia akademi na usajili na amekuwa mshauri mkubwa wa mabosi wa timu hiyo.

Lakini Wenger ambaye alidumu kwenye kikosi cha Arsenal kwa zaidi ya miaka 20, amesema kama wamiliki wa Liverpool watasikiliza ushauri wa Klopp juu ya kocha mpya hilo litakuwa ni kosa kubwa wamelifanya.

“Hapana hapana. Sifikirii kama hilo linafaa labda wawe wamemuajiri rasmi kama mshauri wa timu, inatakiwa ufanye kazi yako na uache watu wengine wafanye kazi yao, nafikiri timu inafanya kazi vizuri pale kila mtu anapofanya majukumu yake, mwisho wa siku wewe kama mmliki unakuwa unajua kama mambo hayajaenda sawa nani inabidi umuulize.” aamesema Wenger alipofanya mahojiano na BelN Sport na aliweka wazi jinsi yeye alivyowaacha Arsenal wafanye kazi yao ya kutafuta kocha mpya baada yeye kuondoka mwaka 2018 ambapo yeye hakuhusika kabisa.

Hata hivyo, Klopp mwenyewe amewahi kusema kwamba hatahusika kabisa kwenye masuala ya kupendekeza Kocha mpya.

“Hapana, kwa nini nifanye hivyo, inaonekana kama nafanya kazi zote, lakini sio kweli na siwezi kufanya hivyo, mambo yote yaliyotokea kwa zaidi ya miaka minane nikiwa hapa ni kwa kushirikiana.” amesema Klopp

ATE yaipongeza GGML kuwapatia mafunzo ya uongozi Wanawake
Nahodha Tabora Utd aitangazia vita Singida FG