Lydia Mollel – Morogoro.
Mbunge wa jimbo la Kilosa Prof. Palamagamba Kabudi amekabidhi gari ya kusafirishia wagonjwa wa dharula (Ambulance), katika kituo cha afya Magubike Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro yenye thamani ya shilingi milioni 170 ikiwa ni jitihada za serikali katika kuboresha utoaji wa huduma kituoni hapo.
Kituo hicho chenye miaka 58 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966 kinacho hudumia takribani Kata Sita awali kilikuwa kikitumia gari dogo katika kutoa huduma hiyo jambo ambalo lilikuwa halikidhi mahitaji katika kuhudumia wananchi hasa huduma ya mama na mototo.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kapokea ya gari hiyo kituoni hapo mbunge wa jimbo la Kilosa Prof. Palamagamba Kabudi, amemshukuru Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia gari hiyo kwani itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa kata hiyo na maeneo ya jilani.
Aidha Prof. Kabudi amewataka Wananchi na Watumishi kuitunza gari hiyo ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika uboreshaji wa huduma za afya Nchini.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Dkt. Mameritha Basike, amesema ujio wa gari hiyo itasaidia kupunguza vifo vya Mama na Mtoto huku Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho Dkt. Asha Hembela akiishukuru Serikali kwa hatua hiyo ambayo itasaidia kuondoa changamoto za usafirishaji Wagonjwa wa dharula Kituoni hapo.
Abuu Msophe ni Diwani wa Kata ya Magubike ambaye amebainisha mafanikio makubwa walioyapata katika Sekta ya Afya huku Wananchi wa Kata hiyo wakionyesha kufurahishwa na ujio wa gari hiyo kwani itakuwa mkombozi kwao.