Ali Hassan Mwinyi, almaarufu kwa jina la Mzee Ruksa alikuwa ni Rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuanzia mwaka 1985 hadi 1995.
Aliyemtangulia alikuwa ni Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na aliyemfuata ni Hayati Benjamin William Mkapa. Pia alikuwa ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi – CCM, kuanzia mwaka 1990 hadi 1996.
Kabla ya hayo Mwinyi alikuwa ni Rais wa tatu wa Zanzibar baada ya kujiuzulu kwa mtangulizi wake Aboud Jumbe, Januari 1984. Urais wa Zanzibar ulimfanya kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, hivyo aliteuliwa kugombea urais wa kitaifa wakati Mwalimu Julius Nyerere alipoamua kutangaza kutogombea tena kwenye mwaka 1985 akisema anang’atuka.
Kabla hajachaguliwa kuwa Rais, Mwinyi alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Makamu Rais.
Mwinyi alizaliwa Kivure Mei 8, 1925 huko Mkoa wa Pwani wa Tanzania bara, lakini wazazi wake walihamia Unguja alipokuwa mdogo.
Kuanzia mwaka 1933 alipata elimu yake ya msingi na Sekondari kwenye shule za Mangapwani na Dole Sekondari alikohitimu mwaka 1942.
Baada ya masomo ya ualimu aliendelea kwenye Chuo Kikuu cha Durham nchini Uingereza na baadaye alianza kufundisha shule akawa Mkuu wa Chuo cha Ualimu Unguja hadi alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu ya Zanzibar baada ya mapinduzi kwenye mwaka 1963.
Mwaka 1970 alipewa Uwaziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais akaendelea na alifanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Zanzibar, ukiwemo uwaziri wa afya, mambo ya ndani na wa utalii.
Alihudumia pia miaka mitano kama Balozi wa Tanzania nchini Misri na baadaye Januari 1984 aliteuliwa kuwa rais wa Zanzibar baada ya mtangulizi wake Aboud Jumbe Mwinyi kujiuzulu.
Wakati wa Urais wa Mwinyi, sera za Ujamaa zilianza kugeuzwa. Badala yake sera za soko huria zilianzishwa, masharti ya kuingiza bidhaa kutoka nchi za nje yalipunguzwa na uanzishaji wa biashara ya watu binafsi ulihamasishwa.
Mwaka wa 1991, Mwinyi alianzisha Tume ya Nyalali iliyopendekeza kuanzisha mfumo wa vyama vingi nchini. Wakati wa awamu yake kwenye mwaka 1995 ulitokea uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi vya kisiasa nchini Tanzania.
Sera za soko huria za Mwinyi zimeendelezwa chini ya Rais Benjamin Mkapa. Mwinyi mwenyewe, baada ya kustaafu, hakujiingiza katika mambo ya siasa tena.
Rasmi Mzee wetu amelala akiwa ameacha alama katika Taifa la Tanzania, Rais mstaafu wa awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amefariki Februari 29, 2024 saa 11:30 Jioni katika hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alipokuwa anapatiwa matibabu ya ugonjwa wa Saratani ya Mapafu.
Tangu Novemba 2023, alikuwa anapatiwa matibabu huko London, Uingereza na baadaye kurejeshwa nchini kuendelea na Matibabu katika hospitali ya Mzena hadi ambapo amepatwa na mauti.
Akitoa taarifa ya msiba huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametangaza siku saba za maombolezo ambapo kuanzia leo Machi 1, 2024, Bendera zitapepea nusu mlingoti na anatarajia kuzikwa Machi 2, 2024 huko Unguja, Zanzibar.
Ikumbukwe kwamba msemo wake ambao sasa unaleta maana halisi ya maisha alipata kusema kwamba “Maisha ya Mwanadamu ni Hadithi tu hapa Ulimwenguni, ewe Ndugu yangu kuwa Hadithi nzuri kwa watakaoisimulia.”
Tangulia Mzee Wetu – ALLY HASSAN MWINYI.