Rais wa Shirikisho la Soka nchini Cameroon, Samuel Eto’o amesema Rigobert Song sio tena kocha timu ya taifa ya nchi hiyo.

Cameroon waliondoshwa kwenye hatua ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwezi Januari kwa kufungwa na Nigeria waliofika Fainali ya mashindano hayo.

“Hatujafikia malengo yetu na Kamati yetu ya utendaji pamoja na mimi hatuoni kama tutasaini mkataba mpya na Song,” amesema Eto’o.

Song, aliyewahi kucheza pamoja na Eto’o kwenye timu ya taifa ya Cameroon, alipewa jukumu la kuinoa timu ya taifa ya nchi hiyo Februari mwaka 2022.

Akaiongoza Cameroon kufuzu Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Qatar kwa kuiondoa Algeria dakika za nyongeza kwenye mchezo wa mchujo.

Lakini Cameroon walioshinda ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika mara tano waliondolewa kwenye hatua ya makundi ya Fainali hizo pamoja na kupata ushindi dhidi ya Brazil kwenye mchezo wa mwisho.

“Song amefanya makubwa kwenye hii timu,” ameongeza Eto’o. Sasa inabidi tufikirie kuhusu baadae.”

Beki huyo wa zamani wa Liverpool ameshinda mechi sita kati ya 23 alizoifundisha Cameroon.

Mataifa yaungana na UN kulaani mauaji ya raia Gaza
CCM watoa neno kifo cha Mzee Mwinyi