NAUTAFAKARI UZEE.

Umeishi miaka mingi, umeona mengi, umepitia mengi, yapo uliyofaulu na yapo ambayo hukuweza kuyafanikisha, unatazama mazingira uliyoishi ukiwa mdogo huyaoni, mazingira yamebadilika kutokana na mabadiliko ya Kimaendeleo.

Pale palikuwa na miti mlikuwa mkichuma Matunda, pale mlikuwa mkicheza, pale mlikuwa mkikutana, pale mlikuwa mnasoma, pale palikuwa kwa baba, babu, bibi, mjomba, shangazi, jamaa na jirani lakini pale si kwao tena na wengi wa hawa watu hawapo tena, walikwishafariki Dunia.

Ulikuwa na ndugu, marafiki na jamaa lakini mkatawanyika kutafuta maisha sehemu mbalimbali katika Dunia, wengine walifanikiwa na Wengine hawakuweza kufanikiwa.

Ulikuwa na uliosoma nao, lakini mkatawanyika kila mahali Duniani, wengine mnakumbukana lakini mlishahauliana, ulikuwa mtoto, ukawa kijana na muonekano mzuri na mavazi mazuri ya kipindi hicho lakini sasa hivi ngozi ya mwili imesinyaa, nywele zimekuwa na Mvi.

Yale mavazi uliyokuwa unayaona ni ya kisasa kwa zama hizi yanaoonekana ni mavazi ya zamani, zile nyimbo ulizokuwa ukizipenda nazo zimekuwa za kizamani, kama ulibahatika kujenga basi hata Nyumba itaonekana ni ya kizamani Dunia inakuja na mabadiliko ya kimaendeleo kila wakati.

Watu wengi uliokuwa nao karibu wamekwisha aga Dunia, wamefariki, wengine una namba zao za simu lakini kila siku unaumia kuzifuta namba zao kwasababu wameshafariki na kila siku wanazidi kuendelea kufariki, ardhi haichoki kumeza watu, kila siku ni ni safari za kwenda kuzika.

Nguvu nazo zimepungua, akili nayo haifanyi kazi kama ilivyokuwa ikifanya kazi zamani, homa za mara kwa mara (homa za uzee), nazo hazitaki kukuachia nafasi.

Unaishi kila siku ukimeza Dawa na kuhitajika Hospitali mara kwa mara na ukienda Hospitali haupokelewi kama vile ulivyokuwa ukipokelewa ujanani, kwasababu unaenda Hospitali za kawaida ili kumudu gharama lakini pia unahitaji kupata huduma za bure za wazee,

Maisha yako sio yale tena, ulikuwa ukihudumia na kusaidia watu lakini sasa hivi umekuwa ni muhitaji, umekuwa mtu wa kuhitaji msaada wa kulelewa na kuuguzwa.

Huenda hata mwenzi wako wa maisha mke/mume mliyekuwa mkiishi na kufarijiana pamoja naye amekwishafariki, huenda hata baadhi ya watoto wako mwenyewe ambao hukutamani kuona wanakuacha Duniani lakini nao wamefariki.

Kuzika mtoto/watoto kunauma na maumivu yake yanajirudia kila unapokumbuka, huenda uzee umekuja na ulemavu, huoni tena, hutembei, husikii vizuri, husemi vizuri ama umepata ugonjwa wa akili na magonjwa mengineyo.

Kila ukitazama mbele unaona ya kuwa siku zako za kuwepo hapa Duniani si nyingi, unaishi ukijua kuwa muda wowote unaweza kufa kwasababu wengi waliokuzunguka wamekufa, kila kitu ulichonacho unakiacha.

Watoto, mke, ndugu, marafiki, mali na vyote vizuri na vya thamani kwako unaviacha, unakwenda usikowahi kukujua wala kukuona, mwisho wa maisha yako.

Fikra hii inapokaa kichwani inaumiza sana! nimeutafakari uzee mara kadhaa lakini leo nikasukumwa kuandika ili ulimwengu ujue wazee wetu wanakuwa katika hali gani.

Iweni na Jumapili njema,

MUNGU awabariki na kuwalinda!

Ndugu yenu, Ibrahim Jeremiah.

Ujumbe wa Rais Dkt. Mwinyi kwa Rais Dkt. Samia
Wanawake, Watoto wahanga wakuu ajali za majini