Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amekutana na Waziri wa Habari na Utalii wa Somalia, Daud Jama na kulipongeza Taifa hilo kwa kuwa mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Makamba ameihakikishia Jamhuri ya Shirikisho la Somalia dhamira ya Tanzania kuendeleza ushirikiano wake na Somalia na utayari wa kuwasaidia watendaji wake pale watapohitaji msaada katika kipindi hiki cha ugeni ndani ya jumuiya.
Kwa upande wa Somalia, Jama amesema kujiunga na EAC ni miongoni mwa mambo yalikuwa ya vipaumbele kwa Somalia. Kama nchi, na kwamba Somalia iko tayari kujitolea na kutimiza wajibu wake kama mwanachama wa EAC.
Aidha, Jama na Balozi wa Somalia nchini Tanzania, Zahr Hassan wametoa salamu za pole kufuatia kifo cha Rais wa Pili wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi.
Jama na ujumbe wake walifika kwenye ofisi ndogo ya wizara jijini Dar es Salaam wakitokea Arusha, Makao Makuu ya EAC ambapo walikabidhi rasmi Hati za kuridhia Mkataba wa Kujiunga na jumuiya.