Uongozi wa Klabu ya Azam FC umesema upo tayari kumwachia Mshambuliaji Prince Dube kuondoka endapo timu inayohitaji huduma yake italipa dola za Marekani 300,000 sawa na Shilingi Milioni 765 za Tanzania.
Mshambuliaji huyo juzi Jumatatu (Machi 04) aliandika barua ya kuomba kuvunja mkataba wa miamba hiyo ya soka nchini, ikiwa imepita miezi sita tangu asaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo hadi mwaka 2026.
Akizungumza jijini Dar es salaam Afisa habari wa timu hiyo, Thabit Zakaria ‘Zaka za Kazi’ amethibitisha uongozi kupokea barua ya mchezaji huyo akiomba kuvunja mkataba na baada ya kujadili wamekubali ombi hilo, endapo taratibu za kimkataba zitafuatwa.
“Uongozi umeridhia Dube kuondoka lakini anapaswa kufuata matakwa ya mkataba, kwenye kipengele cha mkataba wake li kuvunja au kununua mkataba uliobaki mpaka mwaka 2026, anatakiwa kutoa dola za Marekani 300,000 sawa na Shilingi Milioni 765,” amesema Zakaria.
Zakaria amesema tayari wamemjibu Mshambuliaji huyo au kama kuna timu inayomuhitaji au ni yeye mwenyewe akilipa kiasi hicho cha fedha watamwachia na kuwa huru.
Inaelezwa kuwa mshambuliaji huyo hana maelewano mazuri na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Youssouf Dabo ndio maana anataka kuondoka na alishaanza kuonesha dalili hizo tangu mwanzoni mwa msimu huu akiwa kambini nchini Tunisia.