Aliyewahi kuwa Beki wa Simba SC, Azam FC na Singida Fountain Gate, Pascal Wawa amesema baada ya kuutumikia mpira kama mchezaji sasa ni wakati wa kuanza safari ya ukocha ili kuibua vipaji vipya.
Amesema hayo akiwa kwenye kozi ya ukocha ya Grassroots ambayo inashirikisha washiriki 42 chini ya uratibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya lala (IDFA).
“Baada ya kumaliza muda wangu wa kucheza kama mchezaji sasa ni wakati wa kuingia kwenye hatua nyingine ya maisha yangu kwenye soka kwa kwenda kuibua vipaji vipya kama walivyonishika mkono mimi wakati naanza safari yangu.
“Kusoma kozi ya ukocha hii ilikuwa ndoto yangu ya muda mrefu siku moja nije kuwa kocha naamini inaenda kutimia kwa sababu safari yangu ndio kwanza imeanza na haitaishia hapa,” amesema
Amesema kuwa anauzoefu wa kutosha kwenye soka kwa kupita mataifa makubwa kisoka kama Ivory Coast, Tanzania na Sudan na atatumia mafunzo hayo kwa ajili ya kuendeleza karia yake ya ukocha.