Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, ametembelea Makumbusho ya Mauaji ya Kimbari ya Kigali (Kigali Genocide Memorial) na kuweka taji la maua katika kaburi hilo.
Akiwa kwenye Makumbusho hiyo, Waziri Makamba amewasihi wale wote wenye ushawishi mkubwa na nia njema ama ovu kwa nchi zao kutembelea makumbusho hayo kujifunza umuhimu wa umoja na athari chanya ama hasi zinazoweza kuletwa na matendo yao kwa miaka mingi baadaye.
Takribani miili ya watu 2500 waliopoteza maisha katika Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 imezikwa kwenye kaburi hilo la kihistoria huku kumbukumbu za tukio hilo la kusikitisha zikihifadhiwa na kusimuliwa kwa maandishi na picha jongefu ndani ya kuta za makumbusho hayo.
Waziri Makamba yupo nchini Rwanda kwa ziara ya kikazi ya siku tatu inayolenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.