Klabu ya Singida Fountain Gate imemtangaza Kocha mzawa Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’ kuwa Kocha Mkuu wa kikosi cha klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Singida Fountain Gate imemtangaza Julio, baada ya kuvunja Benchi la Ufundi siku kadhaa zilizopita, kufuatia mwenendo mbaya wa kikosi chao kwenye michezo waliyocheza tangu mwishoni mwa mwaka jana.
Taarifa iliyotolewa na Uongozi wa Singida Fountain Gate imeeleza kuwa, Julio atafanya kazi kwa kushirikiana na Kocha mwingine mzawa Ngawina Ngawina, ambaye alikaimu nafasi ya Kocha Mkuu wakati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Simba SC uliopigwa jana Jumanne (Machi 12), Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Hata hivyo Julio amekabidhiwa Singida Fountain Gate mpaka mwisho wa msimu huu, huku mara ya mwisho kwa kocha huyo mwenye uzoefu wa Ligi Kuu alikuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi la KMC FC ambayo ilimuondoa kocha wake Itimana Thienry.
Julio alifanikiwa kwa asilimia kubwa katika jukumu hilo, kwani aliibakisha KMC FC Ligi Kuu, baada ya kuwa katika mazingira mabaya ya kushuka daraja.