Uongozi wa Klabu ya Singida Fountain Gate FC umefichua mkataba wa Kocha Mkuu mpya Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kwa kusema kocha huyo amesaini mkataba hadi mwishoni mwa msimu huu.
Julio alitambulishwa rasmi usiku wa kuamkia jana Jumatano (Machi 13) baada ya kukamilika kwa mchezo wa Ligi Kuu tanzania Bara kati ya Simba SC dhidi ya Singida Fountain Gate FC iliyokubali kufungwa 3-1, Uwanja wa Azam Complex Chamazi Dar es salaam.
Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, John Kadutu amesema wamechukua uamuzi wa kumtangaza Julio baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo ilipokuwa chini ya Kocha Thabo Senong na msaidizi wake Nizar Khalfan.
“Ni kweli tumempa mkataba wa muda mfupi Julio, hadi mwisho wa msimu huu ili kuangalia mwenendo wa timu katika mechi 10 zilizobaki kabla ya msimu kumalizika baada ya hapo kama tutafanikiwa kubaki Ligi Kuu tutampa mkataba mrefu pamoja na kufanya usajili wa nguvu kuimarisha kikosi chetu,” amesema Kadutu.
Kiongozi huyo amesema mbali ya Julio, pia imembakisha Ngawina Ngawina katika nafasi ya kocha msaidizi na pia wamemchukua Ally Mustapha ‘Bartherz’ kuwa kocha wao wa Walinda Lango.
Kadutu amesema wanaimani kubwa na Julio kutokana na uzoefu wake aliokuwa nao kwenye Ligi ya Tanzania Bara na kutokana na mfululizo wa matokeo mabaya waliyokuwa wakiyapata tangu mwanzo wa mwaka huu wanaamini mchezo ujao dhidi ya Namungo FC watapata ushindi wao wa kwanza.
Singida Fountain Gate ipo nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikikusanya pointi 21 na tayari imecheza michezo 20.