Wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikisimama kwa muda kupisha kalenda ya kimataifa, Tabora United imesema haitarajii kupumzika na watatumia muda huo kusahihisha makosa ili kukwepa kushuka daraja.

Timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, haijawa na matokeo mazuri, kwani mwishoni mwa juma lililopita ilishuhudiwa ikinyukwa mabao 4-2 na KMC na kuwa nafasi ya 13 kwa pointi 21 baada ya michezo 20.

Kwa sasa Ligi Kuu itasimama kwa takribani mwezi mmoja kupisha kalenda ya kimataifa na Tabora United itarudi uwanjani Aprili 14 kuwakaribisha JKT Tanzania.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Henry Mkanwa amesema mapumziko hayo wanapaswa kuyatumia vyema kurekebisha makosa yao kiufundi ili wanaporudi uwanjani wafanye vizuri.

Amesema hawatarajii kwenda mapumziko badala yake wanaenda kuanza na safu ya ushambuliaji ambayo haijawapa kile walichotarajia, sambamba na beki iliyoonyesha kuruhusu mabao.

“Tunaenda mapumziko kwa raha gani, hiki ni kipindi muhimu kwetu kutathimini na kurekebisha tulipokosea, eneo kama straika na beki tunapaswa kuyaangalia kwa jicho la tatu,” amesema Mkanwa.

Kocha huyo ameongeza, kuhusu ratiba ya timu hiyo ikiwamo mechi za kirafiki wanaenda kukaa na uongozi kuweka mipango sawa kuhakikisha wanafanya vizuri na kujinusuru kushuka daraja.

“Mipango mingine ni lazima kukutana na uongozi kuweka mikakati, suala la kushuka daraja ni mapema sana kulizungumza kwa sababu mechi bado zipo na lolote linaweza kutokea” amesema kocha huyo.

Wawa anavyoitazama kesho yake
Singida FG wafichua mkataba wa Julio