Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan jumla ya minada ya kisasa 51 imejengwa nchi nzima, ikiwa na thamani ya Shilingi Bilioni 17.5.
Ulega ameyasema hayo katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, ya kukagua mradi wa ujenzi wa mnada wa kisasa wa Horohoro uliopo Wilayani Mkinga, Mkoani Tanga.
Amesema, “kazi iliyofanyika ni kubwa kwa sababu kwa muda mrefu tumekuwa hatujapata fedha za namna hiyo, tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia kwa maono hata inafikia ndani ya miaka 3 minada 51 kujengwa katika wilaya mbalimbali hapa nchini.”
Aidha, alisema uwepo wa mnada huo mpya wa Horohoro uliopo mpakani, unatarajiwa kuwa chachu ya biashara na kuchagiza uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja wanaoishi karibu na mnada huo.