Kuelekea katika mchezo dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wametamba kuwa hawataingia uwanjani kwa hofu kwani wanaamini wana wachezaji wenye ubora.
Young Africans itachuana na Mamelodi Sundowns Jumamosi (Machi 30) katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, utakaochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Rais wa Young Africans, Mhandisi Hersi Said amekiri ubora wa wapinzani wao kuwa mkubwa, lakini anaamini timu yake itafanya vyema katika mchezo huo na kujiweka katika mazingira mazuri ya kucheza Nusu Fainali.
Hersi amesema ana imani na wachezaji wao kuwa watambana kwa kiasi kikubwa na hawatokuwa na hofu yoyote katika mchezo huo, kwa kuwa lengo lao ni kuutumia vyema uwanja wa nyumbani.
“Tunajua tunakwenda kupambana na timu yenye kikosi kizuri, uwezo mkubwa na uwekezaji mkubwa, hatutaingia uwanjani kinyonge, tutapambana kuhakikisha tunakuwa bora,” amesema.
Hersi amesema malengo yao ya msimu huu yalikuwa ni kufika hatua ya Nusu Fainali, kwa kushirikiana Benchi la Ufundi wanaamini watafanikiwa hilo.
“Kwa kushirikiana na Benchi la Ufundi, tunapambana kuhakikisha tunakaa na wachezaji kwa kuwajenga kisaikolojia, waingie uwanjani wakiwa na ari ya kupambana,” amesema.
Amesema Benchi la Ufundi lilitoa mapumziko ya siku tatu kwa wachezaji ambao hawapo katika timu za taifa na timu ilianza mazoezi jana Jumatano (Machi 19) kujiandaa na mchezo huo.
Young Africans ilifuzu hatua ya Robo Fainali baada ya kumaliza nafasi ya pili katika Kundi D, ikiwa na alama nane nyuma ya Al Ahly yenye alama 12.