Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amemuagiza Waziri wa Ncho Ofisi ya Rais – TAMISEMI kutuma timu
ya watalaamu kufika Wilaya ya Mwanga na kuchunguza matumizi ya fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo.
Dkt. Mpango ameyasema hayo mara baada ya kukagua ujenzi wa Hospitali hiyo akiwa ziarani mkoani Kilimanjaro na kuoneshwa kutoridhishwa na usimamizi wa ujenzi wa hospitali hiyo ikiwemo msimizi wa mradi huo ambaye ni mhandisi wa kilimo kutokuwa na vigezo vya kusimamia ujenzi wa hospitali.
Amesema miundombinu ya hospitali hiyo hairidhishi ikiwemo milango iliyo na viwango vya chini zaidi. Amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kusimamia kikamilifu mradi huo na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.
Akizungumza na Wananchi wa Mwanga, Makamu wa Rais amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuendelea kudumisha amani na utulivu katika eneo hilo, huku akiwataka kuachana na tabia ya kulima dawa za kulevya aina ya mirungi na bangi katika maeneo ya milimani.