Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wameingia kwenye ubia ili kuanza utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa kusambaza umeme kwenye nyumba 5,000 katika kijji cha Msomera, Saunyi na Kitwai B, wilayani Handeni, mkoani Tanga ambapo Mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 48.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema, Mradi huo utakuwa endelevu na kuongeza kuwa licha kuwafikishia Wananchi huduma ya umeme katika vijiji hivyo lakini pia utawaunganisha Wananchi na huduma ya umeme (Wiring) moja kwa moja kwenye nyumba zao bila ya wao kulipia huduma hiyo.

“Nyumba 5,000 zitasambaziwa umeme pamoja na kufanyiwa “wiring”. Lengo la Serikali ni kuhakikisha Wananchi katika vijiji hivyo, mnapata umeme lakini pia mnaishi vizuri na kufanya shughuli zenu za kiuchumi,” amesema Naibu Waziri Kapinga.

Naibu Waziri Kapinga amewaambia, wakandarasi wanaotekeleza Mradi huo kuongeza kasi katika kazi hyo pamoja na kutanguliza weledi (Professionalism) katika majukumu yao.

“Tekelezeni Mradi huu kwa wakati ili Wananchi wapate umeme kwa wakati, tunawategemea mfanye kazi kwa weledi, (Sisi) Viongozi wa Wizara ya Nishati, tupo pamoja nanyi ili kuhakikisha Miradi hii yote, inakamilika kwa wakati,” alisema Kapinga.

Mradi huo mkubwa utatekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupitia mkandarasi, kampuni ya China Railways Construction and Electrification Bureau Group Company Ltd (CRCEBG) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia kampuni yake tanzu ya ETDCO.

Katika mkabata huo, Kampuni ya CRCEBG itajenga miundombinu ya umeme katika maeneo ya Mradi wa ujenzi wa Nyumba 5,000 kwa shilingi bilioni 14.2 ambapo, mkandarasi huyo atajenga umeme wa msongo wa kati wenye urefu wa kilomita 281 pamoja na kufunga mashine umba (Transformer) 190.

Kwa upande wa Kampuni ya ETDCO, nayo itajenga miundombinu ya katika maeneo yaliyobaki ya Mradi huo pamoja na kuwaunganishia Wananchi na huduma ya umeme (Wiring) kwa nyumba hizo 5,000 kwa gharama ya shilingi bilioni 33.8 na kufanya jumla ya shilingi bilioni 48 kwa Mradi wote.

Dkt. Mpango aagiza uchunguzi Hospitali Mwanga
Thibaut Courtois afanyiwa upasuaji