Kikosi cha Simba SC kimewasili salama mjini Cairo, Misri tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mabingwa watetezi Al Ahly.
Simba SC itacheza mchezo huo keshokutwa Ijumaa (Aprili 05) katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, ikiwa na deni la kulipa bao 1-0, baada ya kupoteza mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Ijumaa (Machi 29).
Kikosi cha Simba SC kilianza safari mapema leo Jumatano (Aprili 03), kikiwa na wachezaji 23, viongozi wa Benchi la Ufundi na viongozi wa klabu pamoja na mashabiki 17 ambao wamejilipia gharama zao wenyewe.
Orodha ya wachezaji iliyotolewa na Simba SC Walinda Lango ni Ayoub Lakred, Ally Salim na Hussein Abel.
Mabeki: Shomari Kapombe, Israel Mwenda, David Kameta ‘Duchu’, Mohamed Hussein, Henock Inonga, Che Fondoh Malone, Kennedy Juma na Hussein Kazi.
Viungo: Babacar Sar, Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma, Mzamiru Yassin, Abdallah Hamisi, Saido Ntibazonkiza, Kibu Denis, Luis Miquissone, Clatous Chama na Essomba Onana.
Washambuliaji: Pa Omar Jobe na Freddy Michael.
Katika mchezo huo hiyo, Simba SC inahitaji ushindi kuanzia mabao 2-0 ama 2-1 au 3-2 na kuendelea ili kuweza kutinga Nusu Fainali, ambayo ndiyo malengo yao makuu msimu huu 2023/24.