Kocha Mkuu wa Namungo FC, Mwinyi Zahera amesema ushindi wa Penati 5-3 dhidi ya Kagera Sugar kwenye mchezo wa Robo Fainali wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara, ni ishara nzuri katika kuwania taji hilo.
Ushindi huo uliopatikana baada ya sare ya kutofungana kwenye Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa mwanzoni mwa juma hili, uliifanya Namungo kuwa timu ya kwanza kutinga Robo Fainali ya michuano hiyo ambayo taji lake linashikiliwa na Young Africans.
Zahera amesema alijua mchezo huo ungekuwa mgumu ndio maana aliwaheshimu Kagera Sugar kwa hawana muda mrefu toka wakutane kwenye ligi na hivyo alijua lazima wangeingia kwenye mechi hiyo tofauti.
“Mimi ni kocha lazima nimuheshimu mpinzani wangu, nimefundisha soka kwa kipindi kirefu najua mbinu nyingi, hivyo nilijua ugumu wa mchezo ule ndio maana nikafanya maandalizi mazuri yaliyotupa ushindi,” amesema kocha huyo wa zamani wa Young Africans.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Fred Minziro alisema hayo si matokeo waliyotarajia kwani kikosi chake kilikuwa na nafasi ya kusonga mbele, lakini Penati hazina mwenyewe wamepoteza.
“Ulikuwa mchezo muhimu kwetu, tulihitaji ushindi kuendelea hatua inayofuata lakini malengo yetu hayajatimia tunarudi kujipanga kwa ajili ya kumalizia michezo ya Ligi Kuu Bara,” alieleza Minziro.