Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) imeendelea na jitihada za kuhakikisha usalama wa milki za ardhi unaboreshwa, ili kuchochea maendeleo.
Kupitia mpango huo, kwa Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera takribani vijiji 75 vitanufaika na mradi huo kwa kupangiwa matumizi ya ardhi ambapo mpaka sasa vijiji 40 matumizi yake yamekwishaandaliwa.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa wakayi akifungua mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) wilayani Ngara.
Amesema, ‘‘mipango ya Matumizi ya Ardhi ya vijiji vyetu ni nyenzo ya upangaji inayoainisha matumizi mbalimbali ya rasilimali ardhi kulingana na mahitaji, hali halisi ya kiuchumi na kijamii, uwiano wa matumizi, ili kuongeza tija katika uzalishaji, uhifadhi na matumizi endelevu itasaidia katika kuongeza usalama katika milki za ardhi, kukuza huduma za kiuchumi na kijamii, kuboresha hifadhi ya mazingira na kumaliza migogoro itokanayo na ardhi.’’
RC Mwasa ameongeza kuwa ushirikishwaji unaofanywa hapa unatakiwa kwenda mpaka ngazi ya vijiji kila kiongozi katika eneo lake ahakikishe anasimamia utekelezaji wa mradi huu ikiwa lengo ni kuondoa malalamiko, migogoro ya ardhi pamoja na dhuluma kwa wananchi hivyo tuhakikishe ardhi ya watanzania inalindwa ili kuchochea maendeleo.
‘‘Kwa kupanga matumizi ya ardhi pamoja na kuishirikisha jamii itapelekea kumalizika kwa migogoro ya ardhi na kuchochea maendeleo katika Wilaya ya Ngara’’ ameongezea Bi. Mwasa