Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amewashauri Watanzania kuutumia mwezi mtukufu wa Ramadhan kama jukwaa la kuwaelimisha Wananchi kudumisha upendo, umoja na maelewano.
Shaka ameyasema hayo leo alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, wakati wa mashindano ya kuhifadhi Quraani walioshirikisha washiriki kutoka mkoa wa Pwani na Iringa yaliofanyika katika viwanja vya Msikiti Bomani.
Amesema, siku zote imani za dini zimekuwa zikitumika na kuwa kiungo kinachounganisha watu, hivyo vibaki kuwa mwiko na marufu dini kutumika kuwagawa wananchi aidha kwa madhehebu zao, kanda au kwa makabila yao.
Shaka ameongeza kuwa kila Mtanzania na muumini wa dini yake aelewe kuwa taifa halina dini bali wananchi wake ndiyo wenye kufuata imani za dini na viongozi wa dini wanatakiwa kulisimamia hilo.
“Kila mtanzania nchi yetu inamtambua ni binadamu anayestahili heshima na haki kwa mujibu wa katiba yetu. Taifa letu katiba yake imempa uhuru wa kuabudu bila kuvunja mpaka, Kikitokea chama au kundi chenye lengo la kuvuruga amani na kupandikiza chuki lilaaniwe na jamii ya watanzania,” amesema.
Aidha, Shaka aliwataka viongozi wa dini waendelee na kazi ya kuipika mioyo ya waumini wao huku wakiwahimiza na kuwaeleimisha fadhila na neema za kumuamini Mungu ili waifanye mioyo yao iwe na rutuba ya upendo na kuwajali wenye dini na hata wasio na dini.
“Nawahusia muufanye mwezi huu mtukufu wa Ramadhan uwe jukwaa la uadilifu linalotoa elimu itakayowajengea maarifa waumini na wasio na dini .Viongozi wa dini zote waendelee kuhubiri upendo ndani na nje ya nyumba za ibada. Misikiti na makanisa yaendelee na kazi ya kuelimisha imani na umoja,” alisema.
Naye kadhi wa Mkoa wa Morogoro, Mohamed Masenga amesifu jitihada za viongozi wa serikali katika kuwaunganisha watanzania jambo ambalo nchi imeendelea kuwa na amani, upendo na umoja huku wakishuhudi mipango mbali mbali ya kuletea maendeleo ikifanikiwa.